UKURASA WA 701; Thamani Iliyopo Ndani Ya Kushindwa…

By | December 1, 2016

Utashindwa mara nyingi kuliko utakavyofanikiwa kwenye maisha yako, huu ni ukweli wa maisha ambao ni mchungu lakini hatuwezi kuukwepa. Na ukijaribu kuukwepa utashindwa mara zote na hutafanikiwa kabisa kwenye maisha yako.

Kwa kuwa kushindwa ni sehemu ya maisha, na kwa kuwa utashindwa mara nyingi tu kwenye maisha yako, usipoteze muda wako kufikiria kama utashinda au utashindwa. Badala yake tumia muda huo kuhakikisha unaipata thamani iliyopo kwenye kushindwa.

Ipo hivi rafiki yangu, hakuna kitu kinachotokea kwa bahati mbaya kwenye maisha yako. Kila kitu kinatokea kwa sababu, labda umesababisha wewe mwenyewe, au umejiweka kwenye mazingira yaliyosababisha hicho kilichotokea. Hivyo basi unaposhindwa, siyo bahati mbaya, bali wewe mwenyewe, kwa kujua au kutokujua umetengenezwa kushindwa huko.

Hivyo basi, kwenye kila jambo unaloshindwa, kaa chini na ipate thamani halisi ya kushindwa kwako. Kila unaposhindwa jambo usikimbie tu au usihangaike kutaka kuwalaumu wengine. Bali kaa chini na jiulize wewe una mchango gani kwenye kushindwa kwako. Kisha jiulize ni kipi umejifunza katika kushindwa kwako. Lazima ujifunze kitu katika kushindwa kokote unakopitia.

Hii itakusaidia kujiandaa vizuri baadaye, kuchukua tahadhari na kutokurudia makosa uliyofanya awali. Kila unaposhindwa, chukua jukumu hilo la kushindwa, na hakikisha unakuwa mjanja zaidi baada ya kushindwa kuliko kabla hujashindwa.

Kila kushindwa kuna thamani kubwa sana, ni jukumu lako kukaa na kila hali iliyokushinda na kuhakikisha unaikamua thamani iliyopo ndani yake. Ni lazima utoke na kitu ambacho utakifanyia kazi ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi. Pia tumia kushindwa kama sehemu ya kujijengea nidhamu kwamba siyo kila unachokitaka unakipata kwa muda unaotaka, uvumilivu ni hitaji muhimu la mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.