UKURASA WA 702; Mafanikio Ni Kiasi, Jua Kiasi Halisi Na Acha…

By | December 2, 2016

Katika maisha yetu ya kila siku, kila kitu tunapaswa kufanya kwa kiasi, siyo kidogo na siyo sana, bali kiasi. Kufanya chini ya kiasi tunakuwa ni wazembe na kukosa mambo mazuri kwenye maisha yetu. Na kufanya zaidi ya kiasi tunakuwa wasongo na kuharibu hata kile kizuri tulichokuwa tunataka.

Mafanikio kwenye maisha yetu yanatokana na kiasi, kama tunafanya kwa kiasi, tunaweza kuwa na maisha bora na tunayoyafurahia. Lakini tukifanya chini ya kiasi hatuwezi kufikia mafanikio, na tukifanya zaidi ya kiasi tunaharibu yale mafanikio ambayo tumeyapata.

Kwa mfano, nyundo ni kifaa kizuri na muhimu sana, ambacho tunaweza kukitumia kuingiza msumari kwenye mbao. Nyundo inakuwa na matumizi mazuri kama tutagonga msumari mpaka ukaingia kwenye mbao, halafu tunaacha. Ila kama tutaendelea kuigonga mbao hata baada ya msumari kuwa umeingia, tutaiharibu kabisa mbao. Maana yake hapa tumepitiliza kiasi.

Kwa mfano halisia, ni muhimu sana kupata faida kwenye biashara ambayo umechagua kufanya, lakini unapotaka kukamua faida kwenye kila kitu unachofanya kwenye biashara, unaweza kuwa kwenye hatari ya kuharibu biashara hiyo.

Kusaidia ni kuzuri, lakini kama utasaidia zaidi ya kiasi, unaweza kujikuta unarudi nyuma badala ya kusonga mbele. Kazi ni nzuri ili kufanikiwa, lakini kama unafanya kazi zaidi ya kiasi, na kusahau maeneo mengine muhimu kwenye maisha yako, kazi hiyo itaharibu mafanikio yako.

Ni muhimu sana kujua kiasi sahihi kwetu ni kipi kwa mafanikio yetu, na kwenda na kiasi hicho. Tusizoee kwenda zaidi ya kiasi hicho kwa sababu itaharibu kabisa mafanikio ambayo tumeshayatengeneza. Wengi wanaoshindwa baada ya kupitia mafanikio wanakuwa wamezidisha kiasi kwenye mambo wanayofanya. Utasikia watu wakisema mafanikio yamewapanda kichwani.

Jua kiasi sahihi kwako ni kipi kisha nenda nacho, maisha ni kiasi, kwa mambo yote mazuri na mabaya.

Muhimu; kutafuta na kufuata kiasi kusikufanye wewe uwe mvivu, uache kuweka juhudi kubwa kwa sababu unaogopa kupita kiasi. Jua kiasi na hakikisha unafikia kiasi hiki mara zote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.