UKURASA WA 706; Watu Wanaostahili Muda Wako Na Vitu Vinavyostahili Fedha Zako…

By | December 6, 2016

Muda ni rasilimali muhimu sana kwenye maisha yetu. Ni rasilimali pekee ambayo ikishapotea hatuwezi kuipata tena. Hakuna kitu unaweza kukilinganisha na muda. Lakini cha kushangaza muda ndiyo kitu kinachopotezwa zaidi na watu wengi.

blog-timemoney-600

 

Kadiri unavyofanikiwa, ndivyo watu wengi zaidi watakuwa wanahitaji muda wako. Wengi watakuja na mahitaji ya muda wako, kutaka ushauri wako au kukutaka uwe kwenye shughuli zao.

Hata kama unapenda kiasi gani, huwezi kukubali kila ombi au hitaji la kila mtu. Utajikuta unatumia muda wako kufanya mambo ambayo siyo muhimu kwako na wakati huo pia hayawasaidii wengine.

Unahitaji kuchagua sana watu gani ambao utatumia nao muda wako, lazima uwe mwangalifu sana ni mambo gani unayokubali. Hakikisha unakubali yale mambo ambayo yana maana kwako na kwa wengine pia. Hakikisha muda wako unautumia kwenye mambo ambayo yanaleta mchango mkubwa baadaye. Siyo kila jambo linaweza kuwa na sifa hii, hivyo lazima uchague vizuri na kwa makini.

Unapoendelea kufanikiwa kuna mambo mengi ambayo utaona unaweza kuweka fedha zako. Watakuja watu na mapendekezo mbalimbali, kwamba fanya hivi au fanya vile. Utaona fursa nyingi ambazo unatamani kuweka fedha zako.

Pia wapo watakaokusema kwamba una fedha lakini hujui jinsi ya kuzitumia vizuri. Haya yote yatatokea kila mara kadiri unavyofanikiwa.

Hapa pia unahitaji kuwa na umakini mkubwa katika kuchagua mahali unapowekeza fedha zako. Wekeza fedha zako kwenye vile vitu ambavyo vinakusogeza mbele, vitu ambavyo vina maana kwako na pia unavifahamu vizuri.

Usisukumwe kuweka fedha mahali kwa sababu kila mtu anafanya hivyo, au kwa sababu watu wanakuambia unapitwa. Ni fedha zako, chagua kuziweka mahali ambapo unajua zitatoa matokeo chanya.

Hata katika kutoa msaada, usitoe tu kwa sababu unatakiwa kutoa, bali toa kwa sababu unaona kuna mabadiliko utakayoleta kwa fedha unayotoa.

Vitu hivi viwili, muda na fedha, tumekuwa tunavipoteza kila siku kwa kufanya maamuzi ambayo siyo makini. Anza sasa kuwa makini kwa kuchagua kile ambacho kinastahili muda wako na fedha zako, halafu puuza vingine vyote ambavyo havistahili muda na fedha zako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.