UKURASA WA 709; Usifanye Kabisa Biashara Hii, Ni Kupoteza Muda Wako…

By | December 9, 2016

Rafiki, sipendi kukuambia ni vitu gani usifanye, kwa sababu hiyo ni hasi, badala yake napenda kukuambia ni vitu gani ufanye kwa sababu unakuwa chanya.

Lakini kuna wakati nashindwa kwenda na hilo kwa sababu naona wengi wakipotea kwa kukosa maarifa ya msingi kabisa. Ndiyo maana leo nimechagua kukuambia kitu gani usifanye.

Moja ya vigezo ambavyo watu wote tunatumia kuingia kwenye biashara ni kuangalia je biashara hiyo inalipa? Je ina wateja? Je kuna faida? Haya ni mambo ya msingi sana kwa kila mfanyabiashara makini kuzingatia. Lakini kwenye kuchunguza hayo, wengi hawapendi kujiumiza kwa kuingia ndani zaidi, badala yake wanachukua njia rahisi na njia hiyo ni kuangalia biashara gani inavuma kwa wakati huo.

Wanaangalia biashara gani inaongelewa sana, biashara gani ambayo ni “habari ya mjini” na kisha kuingia kwenye biashara hiyo. Ni kweli hii ni njia rahisi, haikuhitaji ufanye utafiti wa kina kwa sababu kila mtu atakuwa anazungumzia aina hiyo ya biashara.

Sasa rafiki yangu, hii ndiyo biashara hatari zaidi kwako kufanya, na ndiyo nataka kukuambia epuka sana kuingia kwenye biashara ya aina hii.

SOMA; UKURASA WA 708; Wazo Bora Pekee Halitoshi…

Epuka kuingia kwenye biashara ambayo ndiyo habari ya mjini. Epuka zaidi kama unaingia kwa kuwa unaona utapata faida kubwa na ya haraka. Hii ni kwa sababu, kama ambavyo nilishakueleza huko nyuma, biashara inayovuma tayari umeshachelewa.

Naomba niweke hili kwa msisitizo; ukisikia biashara inavuma sana, kwamba ndiyo fursa ya sasa, tayari umeshachelewa. Hii ina maana kwamba wale ambao waliingia kwenye biashara hiyo mapema kabla haijawa ndiyo habari ya mjini, ndiyo watanufaika na kuvuma kwa biashara hiyo kwa sasa. Wale ambao wataingia kwa sababu inavuma, wataishia kupata kidogo au wasipate kabisa.

Sasa ufanye nini rafiki yangu?
kama unataka kuingia kwenye biashara, basi chagua biashara ambayo kweli unaweza kuifanya na unajua upo tayari kuipigania kwa muda bila ya kupata faida kubwa.

Kama utashawishika kuingia kwenye biashara ambayo inavuma kwa wakati huo, basi iwe ni kwamba umeipenda biashara hiyo na upo tayari kuendelea kuifanya hata kama hakuna faida kubwa.

Ila kama unaingia kwenye biashara ambayo inavuma, kwa lengo la kupata faida kubwa na ya haraka, basi jua unaenda kuwanufaisha wengine, siyo wewe. Mpaka unaisikia biashara fulani inavuma, jua umeshachelewa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.