UKURASA WA 711; Njia Ya Uhakika Ya Kujiongezea Kujiamini…

By | December 11, 2016

Watu wana mawazo mazuri sana, ambayo kama wakiyafanyia kazi basi yanaweza kuleta mapinduzi makubwa mno. Watu wana ubunifu mkubwa sana ambao upo ndani yao, na kama wakiutumia basi wanaweza kufanya makubwa.

Lakini cha kushangaza, wengi hawatoi zawadi hizi kubwa ambazo zipo ndani yao. Mwandishi mmoja aliwahi kusema, wengi wanakufa na miziki mizuri ikiwa ndani yao, ikiwa haijachezwa kabisa. Mwandishi mwingine akaandika sehemu yenye utajiri mkubwa hapa duniani ni makaburini. Hii ni kwa sababu watu wengi wanakufa na ndoto zao wakiwa hawajazifanyia kazi. Hivyo kila unapoona kaburi, jua kuna utajiri mkubwa umelala pale. Mwandishi mwingine akaandika ni muhimu ufe mtupu (die empty) kwa kuhakikisha unafanya kila unachosukumwa kufanya. Na mimi nikaandika, ACHA KUIDHULUMU DUNIA, nikakuambia ya kwamba kuna kitu ambacho upo hapa duniani kukikamilisha, na ni wewe pekee unayeweza kukamilisha kitu hiki, hakuna mwingine yeyote anayeweza kama wewe. Sasa usipokamilisha kitu hicho, utakuwa umeidhulumu dunia.

Pamoja na kujifunza hayo mazuri kutoka kwa waandishi mbalimbali, bado watu wengi hawawezi kuchukua hatua. Na nimekuwa napokea maoni ya wengi wanaotaka ushauri juu ya hili, nimegundua tatizo linaanzia kwenye kujiamini. Wengi wanashindwa kujiamini na hivyo kuogopa kuanza kwa kufikiria hawajakamilika au watashindwa. Wengine wanahofia watachukuliwaje na wanaowazunguka iwapo watajaribu na kushindwa.

Sasa leo nakuja na dawa moja tu ya kujijengea kujiamini dawa hiyo ni kuanza kufanya. Anza kufanya kitu kwa hatua ndogo sana. Lakini usifanye tu, bali fanya kwa kutengeneza hatua ndogo zitakazokuonesha ushindi mdogo ambao umeweza kupata. Kadiri unavyopata ushindi mdogo mdogo unaanza kujiamini kwamba unaweza na utapata msukumo wa kuendelea zaidi.

Hii ni kama kumla ng’ombe, huwezi kumweka ng’ombe mzima kwenye sufuria na kumpika, bali unamchinja, unamkata vipande vidogo kisha unamla. Hivyo chochote ambacho unajua unahitaji kufanya, na hapa nazungumzia yale mambo ya kipekee ambayo unataka kuyafanya, yale yatakayoacha alama kwenye jamii zetu.

Anza kufanya sasa, kadiri unavyofanya, ndivyo unavyozidi kujijengea kujiamini.

FANYA.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.