UKURASA WA 719; Njia Ya Kuwa Bora Ni Ngumu, Lakini Nzuri Kusafiri…

By | December 19, 2016

Mara nyingi watu wanapoomba ushauri kuhusu mafanikio kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, huwa wanafikiri kuna muujiza fulani, au siri nzito ambayo kila mtu anaijua ila wao pekee ndiyo hawaijui.

Wanapowaona wengine wakifurahia maisha, na kuweka juhudi kwenye yale waliyochagua kufanya, wanaamini watu hawa wameshaigundua siri ila wao tu ndiyo wamebaki gizani.

Na hili ndiyo limekuwa linapelekea watu wengi kutapeliwa na hata kupotezewa muda, kwa kukimbizana na vitu vipya kila siku, kukimbizana na fursa mpya kila siku, wakiamini fursa hizi zina ile siri ambayo bado walikuwa hawajaijua.

Najua ukweli ni mchungu na wengi hatupendi vitu vichungu, ndiyo maana penye utapeli wowote, lazima kuwe na uongo. Lakini mimi nimechagua kukuambia ukweli, kama utaukubali sawa, kama utaukataa pia ni maamuzi yako.

Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, njia ya kuwa bora siyo njia rahisi, njia ya kuelekea kwenye yale maisha unayoyataka siyo njia rahisi hata kidogo. Lakini pia nikufahamishe kwamba ni njia nzuri kuipita, kwa sababu itakuacha ukiwa bora sana.

Njia hii siyo rahisi kwa sababu inakutaka ufanye vitu ambavyo wewe hupendi kufanya. Inakutaka uamke asubuhi na mapema wakati bado usingizi ni mtamu. Inakutaka usikae kila jioni na marafiki mkipiga soga. Inakutaka usiishi maisha ya kuigiza, ukubali kuonekana wa chini ili kuepuka madeni.

Ni njia ngumu kwa kipindi kifupi, lakini matunda yake ni mazuri sana hapo baadaye.

Najua unajua haya yote, lakini nataka kukukumbusha tena rafiki, maana ukikaa muda mrefu bila ya kujikumbusha, unajikuta umeshaanza kushawishika tena labda kuna njia ya mkato. Au kutokana na kwamba kila mtu anafanya, basi huenda ni kitu sahihi.

Kufanya kazi bora, kuanzisha biashara na kuikuza, kufikia uhuru wa kifedha, kuweza kuwa na manufaa kwa wengine ni vitu vizuri ukishavifikia, lakini njia ya kukufikisha hapo siyo rahisi. Ni lazima uwe tayari kwa safari hii ngumu, ambayo utavuna matunda bora sana baadaye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.