UKURASA WA 721; Usitafute Watu Wa Kuwabadilisha, Bali Tafuta Hawa…

By | December 21, 2016

Watu wanapoingia kwenye biashara, huwa na mawazo makubwa na mazuri sana kibiashara. Ambayo kwenye makaratasi yanaonesha faida na mafanikio makubwa. Ila kwenye uhalisia mawazo hayo ya kibiashara yanashindwa kuleta mafanikio yaliyotarajiwa. Mara nyingi biashara hizi ni zile ambazo zinataka kuwabadilisha watu, waache kuamini kile wanachoamini na kuanza kuamini kitu kipya ambacho kina manufaa makubwa kwao.

Watu wanapopanga kuingia kwenye ndoa, huwa wanakuwa na vigezo vya wenza wao. Wanaweka vigezo na kutafuta mtu anayeendana na vigezo hivyo, ikiwa wanakosa, basi wanaweza kukubaliana na waliyempata, kwa mawazo kwamba atambadilisha kadiri siku zinavyokwenda.

SOMA; Vitu Viwili Muhimu Vitakavyowawezesha Watu Kukuelewa Na Kukuamini…

Pamoja na nia nzuri ya kutaka kuwabadili watu, labda kupitia kazi, biashara au hata mahusiano mengine ya kimaisha, bado ni vigumu sana kuwabadili watu. Wewe kama wewe huwezi kumbadili mtu mwingine hata kama utamlazimisha kwa kiasi gani.

Hivyo badala ya kuingia kwenye kitu kwa kuangalia nani wa kumbadilisha, ingekuwa vyema zaidi kama ungeingia na yule ambaye tayari anaamini unachoamini, huyu mnaweza kwenda pamoja na mkanufaika wote.

Kama ni kwenye kazi au biashara, anza biashara kwa kuwahudumia wale ambao tayari wanaamini kile ambacho unaamini wewe. Wale ambao tayari wanaelekea kule ambapo unaelekea wewe. Safari yako itakuwa na vikwazo vichache kuliko kuchagua watu ambao unataka uwabadilishe, waache kile wanachoamini wao na waanze kuamini kile unachowaletea. Hata kama unachowaletea ni bora, bado mabadiliko ni kitu ambacho watu kwa asili hawakipendi.

Kama unaingia kwenye ndoa, badala ya kukubali kuingia na mtu kwa kigezo kwamba mtabadilishana, ni vyema kukubali kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye tayari anaamini kile unachoamini wewe. Tayari anaelekea kule unakoelekea wewe. Kwa njia hii mtakwenda vizuri pamoja. Lakini kujipa jukumu la kumbadilisha mtu, utakutana na vikwazo kila siku, hata kama amekuahidi mwenyewe kwamba atabadilika. Watu huwa hawabadiliki haraka, na tena mabadiliko yanapotoka kwa wengine, ndiyo wanazidi kuyakataa.

Usianze na watu ambao wanatakiwa kubadilishwa, bali anza na wale ambao tayari mnaendana, na hapo utaweza kutoa huduma nzuri na kufika kule unakotaka kufika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.