UKURASA WA 725; Mchezo Wa Kuahirisha Furaha…

By | December 25, 2016

Sababu namba moja kwa nini watu wengi hawana furaha kwenye maisha ni wao wenyewe kuahirisha furaha zao. Na hili linatokana na namna ambavyo jamii imetudanganya kuhusu maisha na furaha kwa ujumla.

img-20161217-wa0002

Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba wakishapata kile wanachotaka basi watakuwa na furaha. Wakishamaliza masomo yao watakuwa na furaha, wakishapata kazi watakuwa na furaha, wakishaoa au kuolewa watakuna na furaha, wakishastaafu kazi watakuwa na furaha.

Ukiangalia huo mlolongo wote, kikubwa kinachofanyika ni kuahirisha furaha. Wanaweka lengo moja wakiamini wakilifikia watapata furaha, wanalifikia na kugundua bado yapo malengo mengine zaidi. Na hapo ndipo wanaahirisha furaha yao kwa lengo hilo jipya.

Nimekuwa nakukumbusha mara nyingi ya kwamba furaha inaanzia ndani yako, furaha inaanza pale ambapo upo sasa, siyo kwa ulichonacho au kwa ulionao. Ni hapo ulipo kwa namna ulivyo ndipo furaha yako ilipo.

Lakini kwa kuwa jamii inayotuzunguka inatuaminisha kupata vitu fulani ndiyo vinatuletea furaha, tumejikuta tumenunua uongo huu na kuishi maisha yasiyo na furaha na mbaya zaidi tunapata msongo wa mawazo pale tunapokosa kile ambacho tulikuwa tunapigania.

Maisha yapo kwa ajili ya kuyaishi sasa, hapo ulipo sasa, iwe una kazi au huna, unasoma au husomi, una familia au huna. Cha kwanza kabisa ni kuyakubali maisha yako kama yalivyo, kufurahia kwa kitendo tu cha kuwa hai. Halafu ndipo unapoweza kuweka mikakati ya kuyabadili maisha yako, huku ukiendelea kuwa na furaha.

Kwa vyovyote vile usiahirishe furaha yako leo kwa chochote unachofikiria kufanya kesho. Kwanza huna uhakika wa hicho unachotaka na una kila sababu ya kuwa na maisha yenye furaha sasa.

Popote unaoitaka kufika, lazima uanzie hapo ulipo sasa, na ukishakuwa vizuri hapo ulipo, ndiyo unaweza kuchukua hatua sahihi za kwenda mbele zaidi.

Maisha yanapaswa kuwa ya furaha muda wote, na siyo kuweka furaha kama lengo fulani la mbali. Ishi sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.