UKURASA WA 737; Watu Wanakuangalia Zaidi Ya Kukusikiliza….

By | January 6, 2017

Wewe kama mzazi, kiongozi, mwajiri au hata mfanyakazi, kuna namna ambavyo unataka watu wawe, kuna mambo ambayo unataka watu wafanye, kwa sababu unajua ni muhimu kwa mafanikio yao na yako pia.

Hivyo unaweza kuchukua muda wako kuwaambia na kuwahubiria namna wanavyopaswa kufanya na kubadilika.

Lakini kama umewahi kujaribu hili najua jibu unalo, ya kwamba unaweza kuongea sana lakini baada ya hapo hakuna linalobadilika, mambo yanaendelea kama kawaida. Unaweza kuendelea kuongea na kusisitiza lakini unaona bado watu wanaendelea kufanya yale ambayo wanafanya.

Hali kama hii inaweza kukukasirisha na kuona labda watu wanadharau, hawakusikilizi au ukaona kama wameshakata tamaa na maisha yao. Huu siyo ukweli, ukweli ni kwamba hujajua njia sahihi ya kuwafanya watu wachukue hatua unazotaka wachukue. Umekuwa unakazana na njia ambayo haifanyi kazi.

SOMA; Usitafute Watu Wa Kuwabadilisha, Bali Tafuta Hawa…

Ukweli ni kwamba watu wanakuangalia zaidi ya wanavyokusikiliza, hivyo ukiacha kuongea sana na ukaanza kufanya, watu wanaona haraka na wao wenyewe watabadilika. Yaani wenyewe watachagua kubadilika na kufanya yale ambayo ni sahihi.

Kwa mfano kama wewe ni mwajiri au ni bosi kwenye eneo la kazi, unaweza kuwapigia watu kelele sana kuhusu kuwahi kazini, lakini wasitekeleze, na wakawa na sababu nyingi kwa nini wanachelewa, na ukizisikiliza zinaweza kuwa zina mashiko kweli. Sasa hebu wewe anza kuwa unawahi, kila siku unakuwa umeshafika kabla hata ya muda wa kufika wa kawaida, taratibu utashangaa watu wanaanza kuwahi na sababu zinapungua. Kwa sababu mtu anaona aibu kuchelewa kila siku wakati wewe unaweza kuwahi.

Njia hii inafanya kazi kwenye kila eneo, kuanzia kwenye familia, kama kuna tabia watu unataka wawe nayo, usipige kelele sana kuhusu watu kuwa na tabia hiyo, badala yake onesha kwa vitendo, watu watajikuta wanafanya kama unavyofanya wewe.

Kwa upande wa pili wa hili tukumbuke ya kwamba watu wanatuangalia na kufanya kama tunayofanya, hivyo kama tuna uzembe fulani, tutegemee watu nao kuiga uzembe huo, hivyo tuwe makini sana kwenye hilo.

Wewe ni mfano na kielelezo kwa wale wanaokuzunguka, hakikisha unakuwa mfano bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.