UKURASA WA 744; Acha Kucheza Michezo Ya Wengine…

By | January 13, 2017

Maisha ni mchezo mkubwa ambao kuna michezo mingi midogo midogo ndani yake. Kuna michezo ya kazi, michezo ya biashara, michezo ya maisha ya kifamilia na mingineyo.

Sasa kuna ambao wanaingia kwenye mchezo, kwa kuchagua kufanya vile vitu muhimu kwenye maisha, kama kazi na biashara, na kuna ambao wanakaa kuuangalia tu mchezo.

Kwa wale wanaoingia kwenye mchezo, kuna ambao wanacheza michezo ya wengine, kwa kuangalia wengine wanafanya nini na wao kufanya na wapo ambao wanakuja na michezo yao wenyewe.

SOMA; Kitu Pekee Kitakachokuletea Utajiri Kwenye Maisha Yako Ni Hiki…

Kucheza michezo ya wengine ni rahisi, kwa sababu tayari sheria za michezo hiyo zipo na wanachohitaji wao ni kuzifuata tu. Lakini tatizo ni kwamba unapocheza mchezo wa wengine, na kuucheza kama wanavyoucheza wao, kikubwa unachoweza kufikia ni yale matokeo wanayopata wao. Yaani ukicheza mchezo wa wengine, utapata matokeo kama watakayopata wao.

Kama matokeo hayo hayakuridhishi unaweza kuboresha zaidi mchezo huo wa wengine na kupata matokeo mazuri zaidi, lakini ya aina ile ile. Unaweza kupata matokeo mazuri kuliko wengine, lakini siyo matokeo bora kabisa. Hii ni kwa sababu mchezo ni ule ule na unachezwa kwa sheria zile zile.

Matokeo bora yanapatikana pale unapocheza mchezo wako mwenyewe, pale unapokuja na mchezo wako, wenye sheria zako mwenyewe na hivyo kuweza kuucheza utakavyo. Hapa una maamuzi yako mwenyewe ya namna ya kupeleka mchezo huo ili kupata matokeo bora kabisa.

SOMA; Kama Unachagua Mwenyewe, Kwa Nini Uchague Hovyo?

Kama unataka mafanikio makubwa, cheza mchezo wako mwenyewe. Njoo na njia tofauti kabisa za kufanya mambo, zenye ufanisi mkubwa ili uweze kupata matokeo bora. Na weka juhudi kubwa kwenye njia hizo ili kupata matokeo mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.