UKURASA WA 768; Uangalie Uhalisia…

By | February 6, 2017

Katika safari ya mafanikio, kila mtu kuna wakati anakutana na magumu.

Wanaofanikiwa wanaweza kuyavuka magumu hayo na kufanya makubwa. Wanaoshindwa wanazuiwa na magumu hayo na kushindwa kusonga mbele.

Kitu kimoja kinachopima kama mtu atayavuka magumu au la ni namna anavyouchukulia uhalisia.

Wale wanaoshinda wanauangalia uhalisia wanapokutana na magumu. Wanajua kabisa mambo ni magumu, na wanajua hakuna anayekuja kuwatoa pale bali juhudi zao wenyewe. Wanajua ugumu wao siyo jukumu la mtu mwingine ila wao wenyewe.

Ila wale wanaoshindwa wanapokutana na magumu, wanakataa kuuangalia uhalisia. Wanaamua kujidanganya kwa mambo ambayo hayawasaidii. Wanazipata njia za kujidanganya na kutoroka uhalisia wa magumu yao. Wanajiambia kuna watu wanawasababishia magumu hayo, au wanawapa watu wengine majukumu ya kuondoa magumu hayo, labda ndugu au serikali. Wanajidanganya kwamba watu wengine wanapaswa kuwatoa pale walipo, au siyo wao wamesababisha magumu wanayopitia, na hivyo hawajisumbui kuyatatua.

SOMA; Hiki Ndio Unachohitaji Ili Kugeuza Ndoto Yako Kuwa Uhalisia.

Usijaribu hata mara moja kuupa kisogo uhalisia, mara zote uangalie uhalisia, unapokutana na magumu angalia uhalisia. Jua ni nini hasa kinaendelea na hatua zipi muhimu kwako kuchukua.

Na linapokuja swala la mafanikio, uhalisia ni kwamba wewe mwenyewe ndiye mwenye jukumu la mafanikio yako. Wewe mwenyewe ndiye msababishi wa changamoto unazopitia. Na wewe mwenyewe ndiye utakayejitoa hapo ulipo sasa.

Kama matatizo au changamoto kwenye maisha yako ni moto unaowaka, basi uhalisia ni kwamba hakuna anayekuja kuuzima, upo mwenyewe na moto wako, pambana nao.

Lakini pia dhana ya umwenyewe haikufanyi uwe mpweke, badala yake inawafanya watu waone juhudi zako na wawe tayari kukuunga mkono. Ni rahisi kumsaidia mtu aliyechukua jukumu na kupambana, kuliko aliyekaa na kuwalaumu wengine.

Usijaribu kuukimbia uhalisia, mafanikio ni kuukubali uhalisia na kuufanyia kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.