UKURASA WA 771; Mawingu Na Jua…

By | February 9, 2017

Kuna wakati ambapo mawingu yanalifunika jua, jua linakuwepo lakini hulioni moja kwa moja kwa sababu ya mawingu. Hulioni jua siyo kwa sababu halipo, ila kwa sababu mawingu yamelifunika. Na kuwepo kwa mawingu hakulizuii jua kuwa jua, wala hakulizuii jua kutoa mwanga wake. Jua linaendelea kutoa mwanga kama kawaida, ila hauonekani kutokana na mawingu. Sasa uzuri zaidi ni kwamba mawingu hayawezi kulizuia jua muda mrefu, yataondoka au yatayeyushwa na kuwa mvua, na jua litaendelea kuonekana tena, likiangaza mwanga wake kwa wengi.

Hivi ndivyo maisha yako na changamoto zilivyo. Una uwezo mkubwa sana ambao upo ndani yako, kuna vitu vya kipekee ambavyo unaweza kuvifanya na kuna juhudi kubwa sana ambazo unaweza kuwa unaziweka kila siku. Lakini huenda hakuna matokeo makubwa unayoyaona licha ya juhudi unazoweka, huenda zipo changamoto nyingi unapambana nazo kwenye zile juhudi kubwa unazoweka. Hapa ndipo wengi wanapokata tamaa na kuona mambo hayawezekani.

Leo nataka nikuambie ya kwamba, wewe ni jua na chochote kinachokuzuia kufanikiwa kwa sasa ni mawingu tu. Hayatadumu muda mrefu, yataondoka yenyewe au unahitaji kuyayeyusha kabisa. Changamoto unazopitia zinakuzuia kwa muda tu, haziwezi kufanya hivyo kwa muda mrefu, hivyo kama hutakata tamaa mapema, utavuka changamoto hizo na utauona mwanga, utaona mafanikio makubwa, utaona matokeo bora yanayotokana na juhudi unazoweka.

SOMA; Kesho Jua Litachomoza Tena…

Hakuna changamoto yoyote ile ambayo inaweza kukushinda na kukuzuia kabisa kufanikiwa. Hakuna.

Chochote unachoweza kujitetea nacho, kuna watu wamekuwa nacho na bado wamefanikiwa. Kama unajiambia ni elimu, wapo wengi ambao hawakupata elimu na wapo mbali. Kama unasema ni kuanzia kwenye familia ya chini, ni bora ukanyamaza kwa sababu karibu kila aliyefanikiwa ameanzia familia ya chini sana.

Usijisalimishe kwa changamoto au vikwazo, kama jua lingejisalimisha kwa mawingu, na kusema sijisumbui kuwaka tena maana mawingu yananizuia kufikisha mwanga, viumbe wote duniani tungeshakufa. Jua linaendelea kuwaka, iwe mawingu yapo au hayapo. Na wewe pia, endelea kuweka juhudi iwe changamoto zipo au hazipo.

Usikubali kurudishwa nyuma na chochote, waka zaidi, ng’ara zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.