UKURASA WA 773; Kuongeza Mwendo, Punguza Mizigo…

By | February 11, 2017

Chombo chochote kinapokuwa na mizigo mingi na mizito, kinakwenda kwa mwendo wa pole pole ukilinganisha na chombo ambacho hakina mizigo. Kadiri mizigo inavyokuwa mizito, ndivyo nguvu kubwa inavyohitajika kuweze kuendesha mizigo hiyo.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa watu, kama umebeba kilo moja ya mchanga, unaweza kukimbia kwa kasi kubwa. Lakini kama umebeba kilo 50 za mchanga, huwezi kukimbia kwa kasi kubwa.

Kwa kifupi tunaweza kusema ya kwamba kasi yetu kwenye maisha, inapunguzwa na mizigo tuliyobeba. Hivyo kama unataka kuongeza kasi yako kwenye maisha, anza kwa kupunguza mizigo ambayo umeibeba hapo ulipo sasa.

Kama unataka kuyafikia mafanikio ni lazima upunguze mizigo ambayo umeibeba, mizigo ambayo inaopunguza kasi yako ya kuelekea kwenye mafanikio.

Mizigo inayowazuia wengi kufanikiwa ni kama ifuatavyo;

  1. Chuki kwa wengine hasa waliofanikiwa.
  2. Vinyongo kwa wale waliowakosea siku za nyuma.
  3. Wivu kwa wale ambao wameweza kufanya makubwa.
  4. Kupenda kufuatilia maisha ya wengine.
  5. Kupenda kufuatilia habari ambazo hazina maana.
  6. Hofu za kushindwa.
  7. Kulalamika na Kulaumu wengine.
  8. Kutafuta njia ya mkato ya kufanikiwa.

Mizigo hii na mingine mingi kama hiyo, imekuwa kikwazo kwa mafanikio ya wengi, imewarudisha watu nyuma na kuwafanya kushindwa kufika wanakotaka kufika.

SOMA; Cross-Selling Na Up-Selling, Mbinu Mbili Za Kuongeza Mauzo Bila Kuongeza Wateja.

Kwa mfano mtu ambaye ana chuki kwa wengine, hasa kwa wale ambao wamefanikiwa, hawezi kufanikiwa kwa sababu akifanikiwa ataenda kinyume na chuki yake. Na kitu kimoja ambacho watu hawapendi ni kwenda kinyume na kile wanachopenda kwenye maisha. Hivyo kuwa na chuki ni mzigo mkubwa kwako kuliko kwa yule unayemchukia.

Kadhalika kuwa na kulalamika na kulaumu wengine, unachofanya ni kujaribu kumbebesha mwingine mizigo yako, lakini huu unakuwa mzigo mkubwa zaidi kwako. Unashindwa kuchukua hatua kwa kuamini wale unaowalaumu ndiyo wenye mamlaka juu ya maisha yako.

Unachohitaji kufanya kwa sasa ni kutua mizigo yako. Tua mizigo yote ambayo inakurudisha nyuma, ambayo inakufanya ushindwe kwenda kwa kasi. Na kila siku pambana kuyafikia mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.