UKURASA WA 792; Hiki Ndiyo Kinawafunga Wengi Wasilione Hata Tatizo…

By | March 2, 2017

Hivi ulishawahi kumwona mtu ambaye yupo kwenye shida fulani, halafu unaona kabisa ipo njia ya yeye kuweza kutoka kwenye shida ile. Unakazana kumwonesha namna anavyoweza kuondoka kwenye shida ile, ila yeye anaishia kukushangaa wewe, anakuona wewe ndiyo umepotea zaidi.

IMG-20170218-WA0000

Anajiona yeye yupo sawa kabisa, na wewe ndiyo una matatizo. Katika hali kama hiyo unachukua hatua gani? Kwa nafasi kubwa, utaamua kuachana naye, kwa sababu utaona ni kama umechagua kutwanga maji kwenye kinu, unatumia nguvu lakini hakuna kinachobadilika.

Sasa hapo unaona kwa wengine, kwa sababu ni rahisi kuona, ila yapo maeneo ya maisha yako, na wewe uko hivyo. Huenda kuna kitu ambacho wewe kinakupa shida, na wapo watu ambao hakiwapi shida, na wakijaribu kukupa njia bora za wewe kufanya, unawakatalia, unaona njia hizo hazifai. Wewe mwenyewe hujui kama uko hivyo, kwa sababu ya kitu kimoja kinachokupa upofu.

Kuna usemi kwamba samaki hajui kama yupo kwenye maji, mpaka pale ambapo anakuwa ameondolewa kwenye maji. Na wewe kuna maeneo uko hivyo, hujui kama upo pabaya mpaka unapofika pazuri. Huamini kama tatizo ulilonalo linaweza kutatulika, mpaka pale unapolitatua.

SOMA; Watu Wana Matatizo Yao, Hawataki Kusikia Yako….

Kinachokupa upofu kwenye matatizo na changamoto zako ni imani yako. Imani ina nguvu kubwa sana, imani inatengeneza na kuzuia mengi. Chochote unachoamini ndani ya nafsi yako, ndiyo ukweli kwako, hakuna cha tofauti na hicho. Ndiyo maana unaweza kuwa unakosea kabisa, lakini wewe unaona uko sahihi, kutokana na kile unachoamini wewe.

Sasa ninachotaka tujifunze leo rafiki yangu, siyo tuache kuamini, bali tuhakikishe imani zetu hazitupotezi. Na njia moja ya kuhakikisha hilo, ni kuhoji na kudadisi. Chochote unachopambana nacho wewe, kinachokupa changamoto au unapotaka kufika, kwanza jiulize, yupo mtu mwingine ambaye ameshafanya hivyo, kama jibu ni ndiyo basi kwa nafasi kubwa ni kitu kinachowezekana. Na hata kama jibu ni hapana, bado usiishie hapo, bali endelea kuhoji na kudadisi zaidi, mpaka utakapoona njia bora kabisa kwako kufanya.

Nimalize kwa kusema tikisa imani zako mwenyewe kabla hata hazijatikiswa na wengine. Hakikisha unajihoji na kudadisi kila unachoamini, ili kuhakikisha upo upande sahihi.

Angalizo; katika kuhoji na kudadisi, unaweza kufanya kosa moja kubwa sana na likakupoteza kabisa. Kwa mfano kama kuna vitu viwili, A na B wewe unaamini A ni bora, lakini unataka kudadisi wengine wanachukuliaje, sasa ili upate unachotaka, unamwuliza mtu ‘eti A si bora kuliko B eh?’. Unafikiri atakujibu nini? Atakujibu ndiyo, hata kama siyo sahihi kwake, kwa sababu tayari umeshatengeneza jibu unalotaka wewe, na hakuna kitu ambacho watu hawapendi kama kukuangusha, hasa kwenye yale unayoamini. Swali sahihi hapo linapaswa liwe, ipi bora kati ya A na b, na hapo unampa mtu uhuru wa kujibu na kukupa sababu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.