UKURASA WA 803; Wewe Ni Biashara…

By | March 13, 2017

Hapo ulipo, wewe binafsi ni biashara, iwe upo kwenye biashara au umeajiriwa, wewe binafsi ni biashara.

Sisemi wewe ni biashara ili ujiuze, ila nasema wewe ni biashara, ili uweze kujiweka vizuri kibiashara na kuweza kufika kule unakotaka kufika.

IMG-20170218-WA0000

Kitu kimoja ambacho wengi hawakielewi, au hawajawahi kufundishwa na kueleweshwa vizuri ni kwamba kila mtu anauza. Kila mmoja wetu, kuna kitu anauza, iwe unafanya biashara, umejiajiri au umeajiriwa, kipo kitu ambacho unauza. Sasa kadiri unavyoweza kuuza vizuri kile unachouza, ndivyo unavyoweza kupata kile unachokitaka.

Sasa turudi kwako kama biashara,

Watu wengi, wanaohitaji kile unachofanya, wanaanza kukununua kwanza wewe, wanaanza kuridhika kwanza na wewe kabla hata hawajakubali kile wanachotaka kwako. Hivyo basi ili kuhakikisha unapata wengi wa kuchukua kile unachotoa, iwe ni bidhaa au huduma, hakikisha kwanza wanajisikia vizuri kwa uwepo wako.

Na awali kabisa, wanahitaji kujua kwamba wewe upo, hivyo lazima ujitangaze. Lazima uhakikishe wale wanaohitaji unachotoa, wanajua uwepo wako.

SOMA; Viungo Vitatu Vya Biashara Yenye Mafanikio…

Unahitaji kulijenga jina lako kupitia chochote unachofanya, hata kama umeajiriwa. Jijengee sifa fulani ambayo ni ya thamani na wengine wanaweza kuitegemea. Inaweza kuwa umakini wako kwenye ufanyaji kazi, inaweza kuwa kauli zako nzuri, inaweza kuwa kujali kwako zaidi. Kwa sifa hizi watu wanaanza kukujua wewe kabla hawajaijua biashara yako au kazi yako.

Kwa dunia ya sasa, hakuna kitu rahisi kama kujitangaza na kuhakikisha wengine wanajua uwepo wako. Lakini wengi hawatumii nafasi hizi vizuri. Mitandao ya kijamii unayotumia, ni njia nzuri sana ya wewe kujitangaza na watu wakajua unafanya nini.

Pia wapo wale ambao wanaona kujitangaza ni sawa na kujionesha au kujigamba juu ya wengine. Wengi wanaogopa kufanya hivyo kwa kuona wataonekana wanaringa au kujidai. Kama una fikra kama hizi, kuna mahali unakosea.

Unakosea namna unavyojitangaza. Huhitaji kuwaambia watu kwamba mimi ndiyo yule mfanyabiashara bora wa vifaa vya magari kuwahi kutokea duniani, bali unahitaji kuwashirikisha watu maarifa na taarifa zinazohusiana na vifaa vya magari, wapi pa kupata vifaa bora, unajuaje vifaa ni halisi na kadhalika. Pia unawakumbusha na wewe unatoa vifaa vya magari na wapi unapatikana.

Inapotokea mtu kwenye mtandao anauliza swali linaloendana na kile unafanya, mjibu kwa njia itakayomsaidia, na kama utamjibu vizuri, atakutafuta zaidi.

Hakikisha mtandao una taarifa zako za kutosha kwa kile unachofanya, kwa kushirikisha mengi kila siku kuhusiana na unachofanya. Kama mtandao hauna taarifa zako zozote kwa zama hizi tunazoishi, dunia inaweza kukusahau haraka sana.

Wewe ni biashara, hivyo jenga jina lako kibiashara, kuwa na sifa ambazo utazisimamia, ongeza thamani zaidi kwa wengine kwa kila unachofanya, na wengi zaidi watakuja kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 803; Wewe Ni Biashara…

  1. Pingback: UKURASA WA 1098; Kujionesha Na Kuonekana, Namna Unavyopoteza Nguvu Zako Mwenyewe. – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.