UKURASA WA 808; Kukamua Sana…

By | March 18, 2017

Ukikamua chungwa linatoa juisi tamu, ambayo ukiinywa unafurahia. Lakini ukikamua sana chungwa, linaacha kutoa juisi tamu na badala yake linatoa maji machungu.

IMG-20170307-WA0003

Ukimkamua ng’ombe unapata maziwa, ambayo unaweza kunywa au kutumia kwa aina nyingine kama chakula. Lakini ukimkamua ng’ombe sana, anaacha kutoa maziwa na badala yake anatoa damu.

Hata wewe binafsi, ukiweka kazi, unazalisha matokeo bora na mazuri, lakini ukiweka kazi kupitiliza bila ya kupumzika unaanza kufanya makosa kwenye kile unachofanya.

Ni sheria ya asili kwamba kila kitu kifanywe kwa kiasi, kulingana na kiasi kinachowezekana. Chochote kinachozidi kiasi kinakuwa siyo kizuri tena na kinaleta madhara.

Changamoto ni kujua mwisho wa kiasi ni wapi na kuacha, na pia kujua namna ya kuongeza kiasi bila ya kuathiri uzalishaji.

Mwisho wa kiasi ni pale kiwango unachopata kwa kukamua kimepungua sana kiasi cha kuwa hakichangii chochote. Kama ni chungwa, umekamua mpaka ukikamua tena hakuna juisi yoyote inayotoka. Kama ni ng’ombe umekamua mpaka ukigusa tena chuchu hakuna kinachotoka. Na kwako binafsi, kiwango ni pale unakazana kuweka juhudi lakini matokeo yanakuwa madogo zaidi ya juhudi ulizoweka. Hapa ndipo pa kujua kiwango kimefikiwa na usilazimishe tena.

SOMA; Tofauti Ya Darasani Na Duniani.

Sasa je tuishie tu kwenye kiwango hicho? Vipi kama tunataka juisi zaidi, maziwa zaidi au kazi zaidi?

Ipo namna ya kuongeza kiwango unachopata wewe, kwa kuhakikisha unakamua wengi zaidi na siyo moja. Ukikamua machungwa mengi utapata juisi nyingi, ukikamua ng’ombe wengi utapata maziwa mengi, na pia ukiwa na watu wengi wanaofanya kazi utapata matokeo makubwa.

Hivyo, badala ya kuhangaika kukamua kitu kimoja, tafuta vingi na uvikamue. Au hata ukiweza kamua kwa msimu, kadiri unavyokuwa na maeneo mengi ya kukamua, ndivyo unavyozidi kuwa na uhakika wa kukamua zaidi na zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.