UKURASA WA 813; Usidhani, Hakikisha Mwenyewe….

By | March 23, 2017

Moja ya vitu vinavyochochea uvivu wa watu ni kudhani. Watu wengi hudhani mambo yanaenda vile wanavyofikiri wao, kumbe yako tofauti kabisa, ni mpaka pale wanapopata matokeo tofauti na waliyotaka, ndiyo wanagundua walichodhani siyo.

IMG-20170303-WA0002

Usidhani kwamba kila mtu amekuelewa kwa kile ulichomwambia, uliza ili uhakikishe mwenyewe. Mara nyingi utakapouliza utagundua watu wamekuelewa tofauti na ulivyosema wewe. Kwa sababu mara nyingi watu wamekuwa wanasikia kile wanachotaka kusikia, na kuona wanachotaka kuona. Uliza na hakikisha mwenyewe.

Usidhani unajua kile ambacho mteja wako anakitaka, hata kama biashara ni yako na huduma unatoa wewe. Bado unahitaji kuuliza ili kujidhibitishia ni huduma ipi itamsaidia sana mteja wako.

Usidhani kila mteja anajua anachotaka, hivyo wewe kumpa tu kile alichokuambia umpe. Wapo wateja wengi ambao hawana uhakika na nini wanataka, kuwauliza kunakupa wewe nafasi ya kukuhudumia vizuri.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kujiongezea Kujiamini…

Usidhani kila uliyemwajiri anajua majukumu yake sawa sawa, hata kama umemweleza, jaribu tena kumuuliza na utagundua kuna kitu hajakielewa sawa sawa.

Muhimu zaidi, usidhani watu wanafikiri kile unachofikiri wewe, au wanahisia kama ulizonazo wewe. Kwa kudhani hivi unaweza kuwapuuza watu na hatimaye kuumiza hisia zao. Kuuliza kutakupa nafasi ya kujua kwa hakika watu wanafikiri na kuhisi nini.

Hata mara moja usidhani, chukua nafasi yako na kujua kiundani, uliza, hoji na jifunze zaidi. Na kadiri jambo linavyokuwa muhimu, ndiyo hupaswi kabisa kudhani.

Wavivu hutumia kudhani ili baadaye wapate watu wa kuwalaumu pale mambo yanapokwenda vibaya. Ili kosa lisiwe kwao, waseme walijua mtu anajua. Sasa wewe usitafute sababu hizi, kwa sababu mara nyingi hata kama kosa ni la mwingine, wewe ndiye unayepoteza zaidi.

Usidhani, jihakikishie mwenyewe, uwe na uhakika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.