UKURASA WA 816; Salama Ni Hatari Zaidi…

By | March 26, 2017

Ninachoendelea kujifunza kwenye haya maisha ni kwamba, unahitaji maarifa sana kuweza kufanikiwa kwenye haya maisha. Na baada ya maarifa unahitaji ujasiri wa hali ya juu sana ili kuweza kufika pale unapotaka kufika. Kwa kukosa vitu hivi viwili, utaishia kuwa ndani ya kundi, kundi ambalo halitaki maarifa wala halihitaji ujasiri, kwa sababu ndani ya kundi kila mtu anafanya kile ambacho kila mtu anafanya. Na hakuna kukosea kwa sababu ndivyo imezoeleka kufanyika.

IMG-20170228-WA0007

Kuna vitu vingi ndani ya kundi ni salama, lakini kwa uhalisia ni hatari zaidi. Lakini ndani ya kundi watu wataambiana ni salama na watakubaliana kwa pamoja na kwenda na hatari ambayo wao wameamua kuona ni salama.

Chukua mfano wa ajira, watu kwenye kundi kubwa la jamii, wanaamini ajira ndiyo njia salama kabisa ya kutengeneza kipato. Na kundi kubwa wanakubaliana kwamba kama huna ajira, basi bado hujawa na maisha. Ndiyo maana mtu anaweza kuhitimu masomo na kukaa mpaka miaka mitatu akisubiri apate ajira ndiyo maisha yaanze, kwa sababu kundi linamwambia, huna ajira, huna maisha, hupo salama.

Lakini ukidadisi na kupata maarifa, utaona wazi kwamba ajira siyo njia salama ya kupata kipato, kwa uhalisia ni njia hatari, kwa sababu unapotegemea sehemu moja tu kupata kipato, unajiweka kwenye wakati mgumu. Na kwa kuwa unachofanyia kazi ni cha mtu mwingine, wakati mwingine unaweza usiridhike na namna mambo yanavyokwenda.

SOMA; Kucheza Salama…

Lakini bado watu wataendelea kuamini kwenye ajira, licha ya kila siku kuwa na malalamiko ya namna zinavyowasumbua. Na hii yote inatokana na ukosefu wa ujasiri wa kuliacha kundi na kuamua kufanya yako. Kwa sababu kuamini na kufanya tofauti na kundi ni kununua vita, kwa sababu kila mtu atakupinga, kila mtu atasema lake. Na hata unapotoka kwenye hatari hiyo ya ajira, unaingia kwenye hatari nyingine kubwa zaidi pale unapokwenda kuanza biashara au kujiajiri.

Vipo vingi sana tunavyoaminishwa ni salama lakini ni hatari, ajira ni mfano mmoja tu. Kila kitu ambacho kundi kubwa la watu linaamini ni salama, anza kukidadisi na kuhoji zaidi, utaona hatari ambayo wengi wameamua wasiione ili waendelee kufanya hicho wanachotaka kufanya.

Sasa wewe usikubali kudanganywa au kujidanganya, jua hatari ipo wapi na namna gani unaweza kukabiliana nayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.