UKURASA WA 818; Zaidi Na Zaidi…

By | March 28, 2017

Kwenye uchumi wa soko huria, unahitaji kuwa makini sana, kwa sababu unasukumwa kufanya vitu ambavyo havina faida kwako ila kwa wengine. Unalazimishwa kuona kwamba hapo ulipo hujakamilika mpaka upate kitu fulani, ambacho ni biashara ya wengine.

IMG-20170314-WA0002

Matangazo ya bidhaa na huduma mbalimbali yanatufanya tujione sisi bado hatuna maisha mazuri na hivyo kukazana kununua vile vinavyotangazwa ili kuwa na hayo maisha mazuri yanayosemwa.

Dhana ya uchumi wa soko huzia ni kuwa na zaidi na zaidi, kwamba chochote ulichonacho sasa hakikutoshi, na furaha inatokana na kuwa na zaidi. Ndiyo maana kila kitu kinawekwa vitu vingi zaidi, ambavyo hata hutavitumia, hata kama utanunua. Utafurahia kununua kitu chenye vitu vingi ambavyo hutavitumia. Na wewe mwenyewe utanunua vitu vingi ambavyo hutavitumia kabisa.

Ni kwenye uchumi huu wa soko huria ambapo utaambiwa wajanja wanakunywa bia fulani, wazuri wanavuta sigara fulani na wenye akili wanatumia mvinyo fulani. Vyote hivi havina faida yoyote kwako, lakini kwa namna vitakavyorembwa na kunadiwa, unaona ni muhimu na wewe uwe mtumiaji.

Hasara kubwa zaidi ya kuishi kwenye uchumi huu wa soko huria ni pale unapoamua kufuata watu wanasemaje. Unakazana kweli kuweka juhudi kubwa, ili upate vile ambavyo umeambiwa ukiwa navyo basi utakuwa na furaha kwenye maisha yako. Unakazana kweli na unavipata, ila sasa unashangaa furaha bado huna. Unachoambiwa ni kwamba unahitaji zaidi na zaidi ili uwe na furaha, hivyo unajikuta kama unafukuza upepo.

SOMA; Salama Ni Hatari Zaidi…

Njia pekee ya kushinda dhana hii ya zaidi na zaidi, ni kujua vitu gani ni muhimu sana kwako. Jua vile ambavyo ni muhimu kulingana na ndoto zako kubwa, pia maadili unayoamini. Halafu fanyia kazi hayo. Pia usiunganishe furaha na chochote unachofanya, furaha haiwezi kuwa zao la chochote unachotaka, unahitaji kuwa nayo kwanza kabla hujapata chochote.

Siyo vibaya kuwa na vitu vingi na vizuri, ubaya unakuja pale tunapofanya hivyo kwa kuamini ndiyo chanzo cha furaha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.