UKURASA WA 832; Tabia…

By | April 11, 2017

Huwa tunazijenga tabia, na baada ya hapo, tabia zinatujenga.

Tabia ni sawa na uzi mwembamba ambao unaweza kuukata bila shida ukiwa mmoja. Lakini kila siku unajisokotea uzi huu taratibu, unapokuja kustuka umeshajisokota mwili mzima na huwezi tena kuukata.

IMG-20170303-WA0002

Hakutakuwa na kelele yoyote kwamba sasa unaanza kutengeneza tabia, bali utaanza kufanya jambo leo, halafu utalifanya tena kesho, na kesho kutwa, mwishowe unajikuta unafanya bila hata ya kujiuliza. Baada ya hapo inakuwa vigumu kwako kuacha kufanya, na hapo unakuwa tayari umeshajijengea tabia.

Hivi ndivyo watu wanavyokuwa wezi, waongo, matapeli, walevi, wazembe, wachapa kazi, waliofanikiwa na kadhalika. Kila kitu kinaanza na tabia, baada ya hapo maisha yetu yote yanafuata zile tabia ambazo tumeshajijengea.

Sehemu ya kwanza; unajengaje tabia nzuri kwako?

Vile vile unavyojenga tabia yoyote, kwa kuanza kidogo kidogo na kurudia kila siku na kila mara.

Kama unataka kujijengea tabia ya kuamka mapema kila siku, anza kuamka mapema na fanya hivyo kila siku, usiache hata siku moja.

Kama unataka kujijengea tabia ya kuandika, anza kuandika kila siku, na isipite siku hujaandika.

SOMA; Tabia Mbili Kwa Kila Mjasiriamali Kuwa Nazo.

Kama unataka kuongeza ufanisi, kutumia muda vizuri na hata kuongeza uzalishaji kwenye kazi zako, chagua kitu utakachofanya kila siku kwenye kazi zako. Kiwe na matokeo chanya na haijalishi ni kidogo kiasi gani.

Chochote unachotaka kiwe tabia kwako, kifanye kila siku na kifanye muda fulani, akili yako itahusisha muda na mazingira na kile unachofanya.

Sehemu ya pili; unavunjaje tabia ambazo huzitaki?

Vile vile kama ulivyozijenga, usitegemee useme siku moja sitaki tena hii tabia na ukaondokana nayo kabisa (labda kama umejitoa kweli).

Unachohitaji kufanya ni kuacha kufanya kidogo kidogo, kile ambacho tayari umeshazoea kufanya. Wakati mwingine fanya kwa mvurugo, badili muda na mazingira unayofanya. Utavunja ule mnyororo wa tabia na kuanza kuachana nacho.

Pia jiwekee njia za kujikumbusha kuhusu kuacha tabia hiyo. Unaweza kujiunga na wengine ambao wanapanga kuacha tabia hiyo, au kuwaambia watu kwamba unaachana na tabia fulani na wao wawe wanaangalia mwenendo wako. Kwa njia hii unalazimika kufanya hata kama hujisikii kufanya.

Tabia ni kitu ambacho unachagua mwenyewe, usikubali kuwa na tabia ambazo zitakutesa. Weka juhudi kujenga tabia zenye manufaa kwako, na vunja tabia zisizokufaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.