UKURASA WA 841; Lawama Na Kukosolewa…

By | April 20, 2017

Wakati mwingine kinachowapa watu hofu ya kufanya siyo kushindwa, bali lawama na kukosolewa. Wakati mwingine watu wanaacha kufanya ili kuepuka lawama, iwapo mambo yatakwenda tofauti na watu walivyotegemea. Na pia watu wanahofia kukosolewa na wengine kwa namna watakavyofanya.

IMG-20170217-WA0004

Lawama na kukosolewa ni vitu ambavyo unapaswa kujifunza kuishi navyo, kwa sababu hutaweza kuvikwepa kwenye maisha yako. Mtu mmoja alipata kusema; kuepuka kukosolewa, usiseme chochote, usifanye chochote na usiwe yeyote. Lakini alisahau kwamba hata kwa kutokufanya chochote bado watu watakukosoa na kukulaumu.

Kwa kuwa hatuwezi kukwepa hayo, inabidi tuchague lawama gani tupo tayari kuzipokea, na ukosoaji gani hatutaujali kabisa.

Katika jambo ambalo ni muhimu sana kwako kufanya, na unajua kuna watu litawasaidia, na una msukumo mkubwa ndani yako wa kulifanya, lifanye. Pamoja na wachache ambao watasaidika, watakuwepo ambao watalaumu kwa namna umefanya. Hawa wachukulie kama walivyo na achana nao, weka nguvu zako kwa wale ambao kile unachofanya kinawasaidia. Hata kukosolewa, hawatakosekana watakaokuambia ungefanya hivi au vile, watakaokuambia umekosea hapa au pale. Wewe fanya kile muhimu kwa wale ambao wanajali.

SOMA; Njia Bora Kabisa Ya Kulalamika Ni Hii.

Nimekukumbusha hili rafiki, ili usije kuacha kufanya kwa kuogopa lawama na kukosolewa. Watu watakulaumu kwa vyovyote vile, watakulaumu ukifanya na watakulaumu usipofanya. Pia watakukosoa ukifanya na watakukosoa usipofanya. Hivyo kipimo chako cha ufanye au usifanye kisiwe ni lawama kiasi gani utakwepa, bali kiwe ni muhimu kiasi gani kwako kufanya jambo hilo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.