UKURASA WA 848; Mteja Hatakuonea Huruma…

By | April 27, 2017

Unaweza ukatumia muda, nguvu na rasilimali zako nyingi katika kuifanya biashara yako kuwa bora zaidi, lakini kama kile unachofanya hakiongezi thamani kwa mteja, mteja hatahangaika na wewe, atakuacha na kwenda anakopata thamani anayotaka.

IMG-20170218-WA0003

Ni muhimu sana kulijua hili kwa sababu nimekuwa naona watu wanawalalamikia wateja, kwamba wateja hawana shukrani, kwamba wamefanya kila kitu lakini wateja hawawaelewi.

Sikia rafiki, mteja anaelewa lugha moja tu, kuna nini kwa ajili yangu, basi, hayo mengine hayana msaada kwake. Mteja ana matatizo, mteja ana mahitaji, anachotaka ni kutatua matatizo yake na kutimiza mahitaji yake.

Hajali kama wewe ndiyo mtu wa kwanza kuanza biashara hiyo, hajali kama umelala njaa kwa kujenga biashara yako, hajali kama una teknolojia ya kisasa kabisa katika kufanya biashara yako, wala hajali kama siku zijazo mambo yatakuwa bora zaidi. Mteja ana mahitaji sasa, ni ama umpe anachotaka aendelee kuwa na wewe, au ushindwe kumpa na aende kule anakoweza kupata anachokitaka.

Kama unasema wateja hawana huruma, wateja hawana shukrani, jua kuna mahali umepoteza. Jua kuna mahali umesahau kipaumbele cha biashara yako ni nini. Kumbuka kipaumbele chako, vaa viatu vya mteja wako, na hakikisha unamtimizia kile anachohitaji.

SOMA; Usimpe Mteja Majukumu Ambayo Siyo Yake….

Mwisho nikukumbushe mteja hakufunga ndoa na biashara yako, hamkupeana ahadi ya kufa na kuzikana, hata kama kuna mkataba mliwekeana, bado unaweza kuvunjwa kama watu hawaridhishwi na wanachopata. Hivyo beba mzigo wako mwenyewe, weka juhudi, toa kinachohitajika, nenda hatua ya ziada na kamwe usitegemee huruma za wateja wako. Maana kwa namna wafanyabiashara walivyo wengi, mteja hana hata huo muda wa kuwa na huruma na wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.