UKURASA WA 855; Inayochukua Muda Ni Hatari Zaidi…

By | May 4, 2017

Mtu akiamka asubuhi, na ghafla akagundua anaharisha damu, atakimbilia hospitali mara moja. Kuharisha damu ni tatizo linaloonekana haraka. Lakini iwapo mtu huyu ataamka tu na tumbo likawa linauma na kuacha, hatakuwa na haraka, au kapata choo kimoja chenye rangi isiyoeleweka, ataendelea kusubiri. Inaweza kwenda hivyo kidogo kidogo, mpaka siku anakuja kwenda hospitali, anakuta ugonjwa ni mkubwa na hauwezi kutibiwa tena.

IMG-20170218-WA0000

Ukiamka asubuhi na kukuta bati la nyumba limeezuliwa, utaweka bati jingine haraka. Lakini iwapo patakuwa na tundu dogo linalovuja, hutakuwa na haraka sana ya kubadili. Lakini kadiri siku zinavyokwenda, tundu lile linaweza kuleta maafa makubwa kuliko ulivyokuwa unafikiri.

Ninachojaribu kukuonesha hapa rafiki, ni namna gani tunaweza kuchukua hatua kwa mambo yanayoonekana wazi, na kuzembea kwa mambo ambayo hayaonekani wazi lakini ni makubwa.

Nimewahi kusema tena, hakuna mtu anaamka asubuhi na kujikuta kwenye madeni ya mamilioni, bali madeni hayo anayatengeneza taratibu, laki hapa, laki mbili pale na kadhalika. Pia hakuna mtu ambaye anaishiwa kila kitu kwa wakati mmoja, bali anakuwa anaishiwa kidogo kidogo, mpaka anastuka hana tena kitu.

Hivyo basi rafiki, kitu muhimu sana kufanya ni kujua kila tunachofanya, na kujua hata pale mabadiliko kidogo sana yanapotokea. Tusiyapuuze tu na kuona ni kitu kidogo, ambacho kitapita. Jiridhishe hasa kuhusu mabadiliko hayo na yajue nje ndani, ili uweze kuchukua hatua sahihi kwako.

SOMA; Umasikini Wa Muda…

Kitu chochote kinachochukua muda mrefu kuonekana wazi, huwa kinakuwa hatari sana. Hivyo kusubiri mpaka vitu viwe wazi, utakuwa umechelewa na kukosa nafasi ya kuchukua hatua. Chochote ambacho hakiendi sawa, hata kama ni kidogo kiasi gani, kinastahili kuangaliwa kwa undani.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.