UKURASA WA 860; Kitu Kimoja Kilichosababisha Yote…

By | May 9, 2017

Jambo lolote linapotokea, ni kawaida kwa watu kutafuta kitu kimoja kilichosababisha yote. Yaani kile kimoja ambacho ndiyo kisababishi.

Iwe ni jambo baya au zuri, mfano inapotokea ajali, kila mtu hutafuta kitu kimoja pekee kilichopelekea ajali ile, labda dereva alikuwa mwendo kasi, au barabara mbovu, au chombo cha usafiri kibovu na kadhalika. Hata katika mafanikio, tunakazana kuangalia kitu kimoja ambacho kimeweza kumtoa mtu chini mpaka juu, kile kimoja tu ambacho kimeleta kila kitu.

IMG-20170217-WA0002

Pamoja na kupenda kwetu kutafuta kitu kimoja kinachosababisha yote, hakuna kitu kama hicho. Linapotokea jambo lolote, kuna vitu vingi sana ambavyo vimehusika mpaka kitu kinatokea. Huwezi kutenga kitu kimoja pekee ambacho ndiyo kimesababisha kila kitu.

Kwa mfano wa ajali, huwezi kusema labda ni mwendo pekee umesababisha ajali, kwa sababu huenda dereva amewahi kuwa na mwendo kama huo, au wengine pia siku hiyo walikuwa na mwendo mkubwa kuliko huo. Unapochunguza kwa undani unakuta vitu vingi vimechangia, vingi mno.

Kadhalika kwenye mafanikio, ni rahisi kuangalia kitu kimoja cha nje na kufikiri ndiyo kimeleta kila kitu, lakini siyo kweli. Ukisema ni juhudi kwenye kazi pekee, wapo wengi wanaweka juhudi kubwa sana, lakini hawapati hayo mafanikio.

SOMA; Tatizo Sio Fedha, Tatizo Ni Wewe.

Hii ni ngumu kufikiri na kuelewa, ndiyo maana naileta kwako wewe kama mwanamafanikio, ujifunze kuchimba ndani zaidi ili kuona kile ambacho wengi hawaoni. Kuwa tayari kuona vile ambavyo vitapingana na unachotaka kuona, ili uweze kufanya maamuzi sahihi kwako na kwa wengine pia.

Umepata hasara kwenye biashara yako, usikimbilie kuangalia kitu kimoja, chimba ndani, utaona mengi zaidi. Kila kitu unachopitia, usikimbilie kukubaliana na kile ambacho kila mtu anaona, wewe angalia ndani zaidi, chimba zaidi na utaona mengi na hivyo kuweza kufanya maamuzi sahihi zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.