UKURASA WA 865; Vitu Ambavyo Hatujui Kama Hatujui…

By | May 14, 2017

Kuna vitu ambavyo tunavijua, na vipo vitu ambavyo hatuvijui. Hii ni kwenye maeneo yote ya maisha yetu, kuanzia kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla.

Katika vile ambavyo hatujui, yapo makundi mawili pia.

Kundi la kwanza ni vile vitu ambavyo tunajua hatujui. Yaani hatujui, lakini tunajua ni kipi hicho hatujui. Vitu hivi tunaweza kuvifanyia kazi, tukavijua na tukawa bora zaidi.

Kundi la pili ni vile vitu ambavyo hatujui kama hatujui. Yaani vitu hivi hatuvijui, na pia hatujui kama hatuvijui. Vitu hivi ni giza kwetu, na hatuwezi kufanya juhudi ya kuvijua kwa sababu hata hatujui kama vipo au vinawezekana.

Sehemu kubwa ya vitu vinavyotukwamisha tusipige hatua, ni vitu hivyo ambavyo hatujui kama hatujui. Kwa kuwa vitu hivi ni giza kwetu, hatuwezi hata kuweka juhudi yoyote. Hivyo tunakwenda tukiona mambo yapo vizuri kumbe kuna muhimu tunayokosa na kujizuia kupiga hatua.

Njia pekee ya kujua yale ambayo hatujui kama hatujui ni kujifunza kila wakati na kukaa chini kutafakari kila tunachofanya. Tunapojifunza tunaona vitu vipya, vitu vinavyowezekana na kuweza kufikiri zaidi. Hata kwa kujifunza kwenye mambo mengine, unaweza kuona namna yanavyowezekana kwenye kile unachofanya wewe.

SOMA; Hatua Sita Za Kuuchuja Ukweli Na Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuukaribia Ukweli.

Kupata muda wa kutafakari na kufikiri kwa kina juu ya kile unachofanya, ni njia nyingine ya kujua yale ambayo hujui kwamba hujui. Unapoiweka akili yako kwenye kile unachofanya, inaweza kukulete uelewa zaidi na kupata ufumbuzi wa yale ambayo yanakukwamisha kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.