UKURASA WA 866; Kinachokuzuia Kuona Mbele… … ni kuangalia nyuma.

By | May 15, 2017

Kuangalia umetoka wapi na ulipotoka watu kama wewe wanaweza au hawawezi kufanya nini.

Kuangalia ulipokosea huko siku za nyuma na kujutia kwa nini ulifanya jambo la hovyo kiasi hicho.

Kuangalia ulipojaribu siku za nyuma ukashindwa, na kujikumbusha kwamba huwezi, hata ukijaribu tena sasa utaishia kushindwa tu.

Yote haya yamekuwa yanakusonga na kila unapojaribu kupiga hatua unashindwa, kwa sababu unaangalia zaidi nyuma na kushindwa kuona mbele. Ni sawa na kuendesha gari huku wakati wote unaangalia kioo kinachokuonesha nyuma badala ya kuangalia mbele. Huwezi kufika mbali, na hapo ni kama hutapata ajali.

Japokuwa ulipotoka ni pagumu, na japo ulifanya makosa makubwa huko nyuma, leo una nafasi nyingine ya kuanza upya na kufanya makubwa kwa siku zijazo. Hakuna anayeweza kurudi nyuma na kubadili yaliyotokea, ila kila mtu anaweza kuanza leo kufanya makubwa na kesho yake ikawa tofauti.

SOMA; Unachotaka Kuficha Ndicho Wanachotaka Kuona…

Hivi ndicho unahitaji kufanya kwenye maisha yako, kuamua kuanza upya, kuamua kusonga mbele. Kuamua kupuuza yale ambayo yamejengeka kwenye akili yako kwamba watu wa aina yako hawawezi kufanya vitu fulani.

Muhimu zaidi, unahitaji kujisamehe kwa makosa uliyofanya huko nyuma, hata kama ni makubwa kiasi gani. Kuendelea kujikumbusha makosa hayo, hakutakusaidia wewe lolote, zaidi ya kuwa mzigo kwako na kukuzuia kupiga hatua kwenda mbele. Jisamehe na acha kujiumiza kwa makosa ya nyuma. Na hata wale ambao walikukosea, pia wasamehe ili uweze kusonga mbele. Kwa sababu kila unapojikumbusha kuhusu wao, unajizuia kusonga mbele.

Usiendelee kujizuia kusonga mbele kwa sababu ya kuangalia nyuma ulipotoka. Badala yake jifunze kwa ulipotoka, ila kazana kwenda mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.