UKURASA WA 872; Mshumaa Usioisha…

By | May 21, 2017

Kila kitu kinachotuzunguka, hasa mazingira asili, yana kitu cha kutufundisha kuhusu maisha. Namna maisha yanavyopaswa kwenda ni kwa sheria za asili, ambazo zinasimamia kila kiumbe hai hapa duniani. Hakuna awezaye kuzipindisha sheria hizi na akafanikiwa kwa muda mrefu. Dunia inamshikisha adabu yeyote anayekiuka sheria za asili.

Mshumaa unawaka na kutoa mwanga, unawamulikia watu, lakini wakati ukifanya hivyo wenyewe unaungua na kupungua au kuishi. Kinachowaka ndani ya mshumaa na nishati iliyopo, ambayo kadiri inavyotoa mwanga ndivyo inavyozidi kuisha.

Jua linatoa mwanga unaomulika dunia nzima, mwanga huu unatunufaisha wote. Lakini huwezi kufika karibu na jua lenyewe, maana inasemekana joto lake ni kali mno. Kuweza kutoa mwanga mkubwa kiasi kile, wa kuitosha dunia nzima, lazima jua liungue zaidi.

Nataka kukuonesha nini hapa rafiki?

Kama ambavyo mshumaa ukiwaka unaisha, na jua linatoa mwanga huku lenyewe linaungua, hivyo na wewe kama unataka kung’aa basi kuwa tayari kuungua. Kama unataka kutoa mwanga kwa wengine, lazima wewe uungue. Siyo kirahisi tu kwamba mwanga utatoka wenyewe bila ya wewe kuumia kwa namna moja au nyingine.

Ndiyo maana mafanikio siyo rahisi, kwa sababu kuna gharama ambazo lazima ulipe, kwenye jambo lolote ambalo unachagua kufanya. Kuna vitu utapoteza ili uweze kung’aa na kuwamulikia wengine. Na hii inafanya iwe muhimu sana kwetu kuchagua ni kitu gani kina hadhi ya kutufanya sisi tuungue. Ni wapi ambapo tupo tayari kuweka juhudi kubwa na hata kuumia. Ni thamani gani ambayo tupo tayari kutoa kwa wengine, kwa gharama kubwa kwetu.

SOMA; Rahisi Kupata, Ngumu Kutunza…

Tujiandae kwa hilo na kuwa tayari kulipa gharama. Miaka 100 ijayo, dunia itakuwa na watu wapya kabisa, lakini hadithi za wachache walioungua kwa ajili ya wengine zitaendelea kuwepo. Je yako itakuwa sehemu ya hadithi hizi zitakazodumu zaidi ya miaka yako? Hilo ni swali la kujiuliza na kujipa majibu kwa kufanya makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.