UKURASA WA 879; Tofauti Ni Falsafa…

By | May 28, 2017

Watu waliofanikiwa wana masaa 24 kwenye siku yao, muda ambao hata wengine pia wanao kwenye siku zao.

Watu waliofanikiwa wanafanya kazi na biashara ambazo wapo wengine wengi pia wanaozifanya, lakini wengi hawajafanikiwa.

Je kuna nini hapa, kipi kimejificha?

Tumekuwa tunaona mengi, kama kuweka juhudi kwenye kazi, kuwa na maono makubwa na kupanga hatua za kuchukua. Lakini bado utakuta wapo watu wanajituma sana lakini bado hawafanikiwi. Wanafanya kazi muda mrefu na wanataka kweli kufanikiwa, lakini haiwi hivyo.

Tofauti kubwa sana, inaanzia kwenye falsafa, ambayo inapelekea mtazamo na hatimaye nini mtu anafanya.

Kwa mfano, wafanyakazi wawili wameajiriwa sehemu moja, wakati mmoja na kipato kinalingana. Mmoja akipokea mshahara wake anawaza matumizi na mambo mengine, akimaliza anasubiri tena mwisho wa mwezi, hivyo falsafa yake ni kufikiria mwisho wa mwezi na matumizi.

SOMA; Tofauti Ya Darasani Na Duniani.

Mwingine akipokea kipato chake anatenga sehemu na kuweka pembeni, anatumia hiyo kuwekeza na kuanza biashara zake za pembeni. Kila akipokea mshahara anaangalia zaidi shughuli zake za uzalishaji na uwekezaji. Huyu yeye hawazi mwisho wa mwezi, bali anawaza miaka mingi ijayo.

Watu hawa wawili, wanaanzia sehemu moja, lakini falsafa zao ni tofauti, njoo miaka kumi baadaye na utakuta kuna watu wawili tofauti kabisa. Utamwonea wivu aliyefanikiwa na kusema ana bahati, na kumwonea huruma aliyeshindwa na kusema ana kisirani. Lakini vyote hivyo havina ukweli, ukweli ni kwamba kuna matokeo ya falsafa ambazo watu walichagua kuziishi.

Je wewe umechagua falsafa ipi? Je itakufikisha wapi? Unawajua wanaoishi falsafa kama yako? Imewafikisha wapi?

Ni muhimu sana kujenga falsafa ya maisha yako ya mafanikio. Soma makala za FALSAFA MPYA YA MAISHA kila siku ili kujenga falsafa imara kwa mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.