UKURASA WA 888; Raha Leo, Maumivu Kesho…

By | June 6, 2017

Kitu chochote kinachokupa raha leo, basi kesho kitakupa maumivu. Hii ni kwa sababu hakuna raha inayodumu kwa muda mrefu, raha ni za muda mfupi pekee.

Kila kinachokupa raha, hicho hicho kinakuja kukupa maumivu.

Na maumivu haya yanakuja kwa pande mbili;

Upande wa kwanza ni kile kile kinachokupa raha kinakuzalishia maumivu. Kwa kutumia au kufanya kile kinachokupa raha, kinazalisha maumivu kwako. Kwa mfano mtu mlevi au mtumiaji wa madawa ya kulevya, mwanzoni wakati anaanza anapata raha, lakini kadiri anavyokwenda, ulevi wake unakuwa maumivu makali kwake. Au utumiaji wake wa madawa unaleta maumivu kwake.

Upande wa pili ni kukosa kile kinachokupa raha, na kukosekana huko kunatengeneza maumivu. Kwa upande huu, kile ambacho kilikuwa kinakupa raha kinakosekana, na hapo yanazaliwa maumivu makali sana. Kwa mfano mtu ambaye alikuwa anapata raha kwa mapenzi ya mtu mwingine, anapoondoka mtu huyo hubaki na maumivu. Au hata mtu anapokuwa mteja wa madawa ya kulevya, asipoyapata anakuwa kwenye maumivu makali.

Suluhisho ni furaha na siyo raha.

Suluhisho la kuepuka maumivu, ni kutengeneza furaha, na siyo kutafuta raha. Elewa vizuri hapo, raha inatafutwa, furaha inatengenezwa. Raha inatoka nje yako, furaha inatoka ndani yake. Hivyo vitu vya nje huwezi kuwa na uhakika navyo, ila vya ndani, ni mali yako.

SOMA; Wamekijua Leo, Walikitaka Jana…

Unapotengeneza furaha, unakuwa nayo muda wote, kwa sababu inaanzia ndani yako. Huhitaji chochote au yeyote ili uwe na furaha, unachohitaji ni kujikubali na kuamua kuishi, kwa kufanya yale ambayo ni muhimu kufanya.

Usikimbizane na raha za nje, hazina mwisho na kibaya zaidi zinakuletea maumivu. Tengeneza furaha ya ndani, na utakuwa nayo milele na maisha yako yatakuwa bora na yenye mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.