UKURASA WA 892; Chukua Hasara, Nawa Mikono, Songa Mbele….

By | June 10, 2017

Safari ya mafanikio siyo rahisi, haijawahi kuwa na haitakuja kuwa. Ni mchakato wenye changamoto nyingi sana. Nyingine zinaweza kutokana na watu ambao walipaswa kutekeleza majukumu yao kama mlivyokubaliana, lakini wasifanye hivyo. Na hii kupelekea wewe kupata hasara au kupoteza zaidi.

Inapotokea hali hii, watu wengi hukimbilia kuwachukulia hatua wale ambao wamewasababishia hasara au kuwakosesha kile ambacho walipaswa kupata.

Labda ni mkataba umeingia na mtu wa kukamilisha jukumu fulani muhimu. Lakini yeye hakufanya sehemu yake, na hivyo kuwa amekosea. Unaweza kuona una haki kabisa ya kumshitaki ili upate kile unachostahili kupata.

Lakini sasa, zoezi hilo la kumshitaki na kumfuatilia mpaka upate kile unachotaka, linaweza kuchukua muda wako mwingi kiasi cha kupelekea wewe kushindwa kufanya shughuli zako vizuri. Hivyo unakuwa umepoteza kile ulikuwa unategemea, na sasa unapoteza muda, fedha na hata nguvu zako katika kumfuatilia mtu huyo.

Kwa nje hilo linaweza kuonekana ni jambo sahihi kufanya. Lakini kwa ndani siyo jambo sahihi, ni jambo la hovyo kwa sababu unapoteza zaidi.

Hivyo, badala ya kukazana kupoteza zaidi, unapokutana na hasara uliyosababishiwa na wengine, kubali hasara, nawa mikono na songa mbele.

Kubali hasara, kwa sababu umeshaipata, na kuikataa kutakutengenezea hasara zaidi, kwa sababu utapambana kupata unachotaka, na hapo kupoteza zaidi.

SOMA; Hasara Ya Kutokufanya Maamuzi Ya Maisha Yako…

Nawa mikono kwa kujitoa kwenye ile hali iliyokusababishia hasara. Kama ni makubaliano ulikuwa nayo na mtu, achana na makubaliano hayo.

Songa mbele kwa kutofanya tena kile ambacho kimekuingiza kwenye hasara. Kama ni mtu basi usifanye naye kazi tena, kwa sababu watu wasumbufu wataendelea kuwa wasumbufu.

Chagua kufanya kazi na watu waaminifu na wanaojali kile unachofanya kazi. Kama utakosea na kujikuta umefanya kazi na watu wasio waaminifu, jitoe haraka kama umestuka kabla ya hasara. Na kama ni baada ya hasara, basi kubali hasara, nawa mikono na songa mbele.

Maisha yana changamoto, muda ni mchache na nguvu zina kikomo, usipoteze kwa mambo yasiyo na tija.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.