UKURASA WA 896; Acha Kutorokea Kwenye Vitabu…

By | June 14, 2017

Kusoma vitabu, au kujifunza ni hitaji la msingi kabisa la mafanikio yetu. Hatuwezi kufanikiwa kama tunafanya mambo yale yale na kwa uelewa ule ule. Tunahitaji kujifunza mambo mapya na njia bora wanazotumia wengine kuwa bora zaidi.

Na hapa ndipo umuhimu wa vitabu unapokuja. Ni muhimu sana kusoma vitabu, vya aina mbalimbali. Vinavyohusu kile unachofanya, vinavyohamasisha na hata vinavyokupa changamoto ya kufikiri zaidi.

Lakini kusoma kitabu pekee siyo mafanikio. Kitabu kinakupa mwanga tu, wakati mwingine kitabu kinakufungulia ujinga wapo. Kuna vitu hujui, lakini hujui kama hujui. Sasa unaposoma kitabu ndiyo unagundua kumbe vipo vitu vingi kiasi hicho huvijui? Na hapo ndipo unapohitaji kujifunza zaidi na zaidi.

Ukisoma kitabu kimoja mpaka mwisho, ni lazima utajikuta kuna vitabu vingine zaidi unapaswa kusoma, mara nyingi siyo chini ya vitabu vitano.

Ninachotaka kukukumbusha leo rafiki ni sehemu ya vitabu kwenye mafanikio yetu. Ni muhimu sana, lakini siyo sehemu pekee. Pamoja na kusoma vitabu, bado tunahitaji kuweka kazi, tena siyo ya kitoto. Tunahitaji kuweka kazi kubwa ili kuweza kufanya makubwa na kupata matokeo bora.

SOMA; Unapata Wapi Muda Wa Kujisomea Na Unapataje Vitabu Vya Kujisomea?

Kitabu ni mwanga tu wa kutuonesha wapi tunapaswa kwenda, juhudi zipi tunapaswa kuweka na mbinu zipi ni bora. Baada ya hapo ni jasho la mwili na akili katika kufanya ili kupata matokeo tunayoyataka kweli.

Imekuwepo tabia ya watu kutorokea kwenye vitabu, yaani kutumia vitabu kama njia ya kutoroka kufanya. Watu hawa hujiambia bado hawajawa tayari na hivyo kuendelea kusoma vitabu mpaka wajione wameiva. Wapo wengine pia wanapoanza kufanya na kuona mambo ni magumu, wanarudi kusoma vitabu. Au katikati ya kufanya, anapoona kitu ni kigumu, anatoroka kidogo na kusoma kitabu, au hata makala.

Nasisitiza sana usome vitabu na mengine mazuri kila siku, ila usitumie kama njia ya kutoroka kufanya kazi ngumu iliyopo mbele yako. Lazima kazi hiyo ifanywe na lazima ifanywe na wewe. Kuikimbia kwa kusoma vitabu wakati ambao ungepaswa kuwa unafanya, hakutaiondoa kazi hiyo. Badala yake ni kujichelewesha kufikia mafanikio unayotaka.

Soma vitabu, na weka kazi ya kutosha. Unapokutana na ugumu usikimbilie kitabu, badala yake weka kazi. Unaweza kwenda kwenye vitabu kujifunza zaidi, lakini hakikisha kazi unafanya na changamoto unatatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.