UKURASA WA 922; Kupata Na Kupoteza…

By | July 10, 2017

Kwa hali ya kawaida, tunategemea kinachopotea na kinachopatikana, kiwe na uzito sawa. Kwamba kama unapoteza mbuzi mmoja, kuwe sawa ila kwa kinyume na kupata mbuzi mmoja. Yaani huzuni ya kupoteza, iwe sawa na furaha ya kupata, kitu kile kile chenye thamani ile ile.

Lakini kwa saikolojia ya binadamu iko tofauti kabisa. Tunahofia zaidi kupoteza kuliko tunavyotaka kupata. Yaani kwa mfano, kukiwa na fursa ya kutengeneza shilingi elfu moja, na hapo hapo kuna nafasi ya kupoteza laki moja, hatutachukua hatua. Kwa sababu kupoteza kunaumiza sana, hakuwezi kufidiwa na kupata.

Kwa thamani ile ile, tunaogopa zaidi kupoteza kuliko tunavyohamasika kupata.

Sasa unaweza kutumiaje hili kwenye mafanikio?

Badala ya kujipongeza kwa kufikia lengo fulani ulilojiwekea, jiadhibu kama hutalifikia. Kwa sababu adhabu au kupoteza kunaumiza zaidi, utasukumwa kufanya, kuliko ungekuwa umejiwekea zawadi.

SOMA; Siri Ya Kupata Ujasiri Wa Kuuliza Chochote…

Kwa mfano, labda tuseme unataka kufanya mazoezi kila siku, au kuandika kila siku, unaweza kujipa zawadi kwamba kama ukikamilisha hilo utapata kitu fulani unachopenda. Sasa siku ukiwa na kasababu kadogo, utaacha kufanya mazoezi, kwa sababu kile unachopata hakikusukumi sana.

Njia nyingine ya kuhakikisha hilo, ni kujiwekea adhabu iwapo utaacha kufanya. Kwa mfano, unaweza kumpa mtu unayemwamini kiasi kikubwa cha fedha, ambacho kitakuumiza kweli, na ukamwambia iwapo utaacha kufanya kile ulichopanga kufanya, basi fedha hiyo aichukue, au hata akaitoe msaada yote. Kwa njia hii, utajisukuma kufanya hata kama una sababu nyingi kiasi gani, kwa sababu kupoteza kunaumiza sana.

Tumia saikolojia yako mwenyewe kujihamasisha kuweka juhudi zaidi ili kuweza kufikia ndoto zako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.