UKURASA WA 937; Usishindane Na Mtu Huyu…

By | July 25, 2017

Kwanza kabisa, msimamo wako muhimu kwenye maisha unapaswa kuwa ni kutokushindana. Usishindane, hakuna jema linalopatikana kwenye kushindana. Hatua bora unayoweza kuchukua ni kuwa tofauti, kujitofautisha na wengine na hata pale ushindani unapokuja kwako kabisa, angalia njia gani ya kuwa bora zaidi.

Lakini hayo yote yanaposhindikana, pale inapokubidi ufanye kitu ili kuondoa ushindani, basi unapaswa kuwa makini kabla hujaamua kufanya hivyo. Unapaswa  kumwangalia kwanza mtu yule ambaye unakwenda kushindana naye.

Iwapo mtu huyu hana chochote cha kupoteza kwenye ushindani huo, kamwe usishindane naye, utaumia sana na hakuna chochote utakachonufaika nacho. Mtu ambaye hana chochote cha kupoteza, yupo tayari kufanya jambo lolote, hata kama litamdhalilisha yeye, ili tu kukukomoa wewe.

Ogopa sana mtu ambaye hana chochote anachojali, huyu atafanya mambo ya hovyo na yatakuharibia zaidi. Ni vyema kujiepusha na watu wa aina hiyo, hata kama itakugharimu katika kufanya hivyo. Ni bora kupoteza kiasi, kuliko kupoteza kila kitu kama yule unayetaka kushindana naye.

SOMA; Kushindana Na Watu Bilioni Saba…

Mara nyingi, mwisho wa ushindani, pande zote zinazoshindana huwa sawa, na huwa chini zaidi ya zilivyokuwa kabla ya kushindana. Sasa unaposhindana na ambaye hana cha kupoteza, ambaye yupo chini kabisa, atakushusha na wewe chini kabisa, ila tu, yeye hataumia kwa sababu tayari alikuwa chini.

Upo usemi unasema kwamba ukipigana na nguruwe, wote mnachafuka matope, ila nguruwe atakuwa anafurahia zoezi hilo, huku wewe ukichafuka na kuwa hovyo zaidi.

Tunatumiaje hili?

Kwenye biashara; usishindane na mfanyabiashara ambaye tayari anapata hasara kwenye biashara yake. Anaweza kuwa anaona biashara inamshinda, na hivyo amekata tamaa hivyo kuibua ushindani utakaowavuruga wengine zaidi. Anaweza kushusha bei ambayo inampa yeye hasara, ili tu kuwavuruga wafanyabiashara wengine, kuwa makini usiingie kwenye mtego wa aina hiyo.

Kwenye kazi; usishindane na mfanyakazi mwenzako ambaye ameshachoka kazi, ameshajua hakuna kipya anachopata na anatamani hata kuondoka kwenye kazi hiyo. Mtu huyu anachotafuta ni kufukuzwa au kuondolewa kazini, ukijichanganya na kuingia kwenye anga zake, mtaondoka pamoja.

Kwenye maisha ya kawaida; usibishane au kutukanana na mtu ambaye kila mtu anamjua ana tabia mbaya au chafu. Kwa sababu huyo hana tena heshima yoyote, atakuwa tayari kutoa maneno yoyote machafu, akijua watu walishamzoea. Ila wewe utakapomjibu maneno machafu, ndiyo utavunja kabisa heshima yako kwa wengine.

Kama tulivyoona kwenye mifano hiyo, mara nyingi wale ambao hawana cha kupoteza, hutengeneza mazingira ya kukutega wewe ili uingie kwenye ushindani na wao, ili wakuangushe na wewe pia. Ona mitego hiyo mapema na hakikisha huingii kwenye mitego hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.