UKURASA WA 938; Nyakati Ngumu Ndiyo Za Kutengeneza Maana.

By | July 26, 2017

Kitu kikiwa rahisi sana, tunakizoea na kuona cha kawaida, hatukipi heshima ya kutosha, thamani yake inakuwa ndogo kwetu na hatukifurahii. Hii ni saikolojia ya binadamu, ambayo usipoielewa vizuri, maisha yako wakati wote yatakuwa magumu, hata ufanye nini.

Watu huwa tunalalamikia ugumu na changamoto mbalimbali tunazopitia kwenye maisha, tunatamani mambo yangekuwa rahisi. Tunatamani kazi zetu zingekuwa rahisi, waajiri wangetuelewa na wafanyakazi wenzetu wangetupa ushirikiano wa kutosha. Tunatamani biashara zetu zingekuwa rahisi, wateja watuelewe na wengine wasianzishe biashara kama zetu.

Hilo huwa halitokei, na pale linapotokea, hali huwa mbaya kuliko wengi wanavyotegemea. Pale kitu kinapokuwa rahisi kufanya, pale ambapo hakuna changamoto, watu hawakui, watu wanarudi nyuma na kuona maisha yanachosha.

Pale ambapo kila kitu ni rahisi, tunaacha kuthamini kila kitu ambacho ni rahisi, na kuanza kutafuta vitu vingine zaidi.

SOMA; Wakati Unapoona Kama Kila Kitu Hakipo Sawa…

Ndiyo maana mara zote nimekuwa nakuambia ufurahie changamoto, yakabili matatizo kwa sababu ni kupitia matatizo hayo ndiyo unakua. Kupitia changamoto ndiyo unajijua vizuri, ndiyo unaweza kufikia uwezo mkubwa ambao upo ndani yako.

Mambo yanapokuwa magumu, ndipo tunapotengeneza maana ya maisha yetu. Ndipo tunapojenga nidhamu, tunapoweka misingi na maadili tunayoyaishi kwenye maisha yetu. Ni nyakati ngumu ambapo tunaona thamani ya vitu, na kuvifurahia pale tunapovipata.

Hivyo rafiki, usitamani mambo yawe rahisi, badala yake taka kuwa bora zaidi ili uweze kupambana na hali yoyote itakayojitokeza mbele yako. Na kumbuka, chochote ambacho hakikuui kinakufanya kuwa bora zaidi. Unazidi kuwa bora kadiri unavyotatua changamoto nyingi zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.