UKURASA WA 951; Kwa Nini Unakazana Kubadili Matunda?

By | August 8, 2017

Iwapo kuna mti umeota shambani kwako, lakini unatoa matunda ambayo wewe huyapendi, unafikiri ukichuma matunda yote na kuyaharibu, msimu ujao utatoa matunda gani? Bila shaka ni yale yale.

Vipi kama ukikata matawi yote yanayotoa matunda, ukasubiri yatoke matawi mapya, na kuanza kutoa matunda, yatatoka matunda gani? Bila ya shaka yoyote matunda utapata ambayo hupendi.

Wote tunajua kabisa na ni sheria ya asili kwamba mti unatoa matunda kwa sababu ya asili yake, kinachotoa matunda siyo matawi wala majani, bali ni asili ya mti, ni mizizi ya mti husika. Hivyo ukitaka kubadili, lazima ubadili kwenye msingi kabisa, ubadili kwenye mizizi. Au ubadili shina, kwa kuleta shina au tawi la ule mti ambao matunda yake unayataka na kupandikiza pale.

Sasa tunajua hili kwa miti na hata wanyama, lakini kwa nini tunalisahau kwetu sisi wenyewe?

Unapofanya biashara yako vile vile, lakini unategemea matokeo mazuri, unakuwa unafikiria nini?

Pale unapoenda kazini kwa mazoea, kufanya kazi kama ulivyozoea, hujitumi, halafu unategemea upate matokeo mazuri, kipato chako kiwe kikubwa, unakuwa unafikiri kwa msingi upi?

Pale unapokuwa na changamoto za kifedha, kipato chako hakitoshelezi, lakini unakimbilia kukopa ili kukidhi mahitaji yako, ni msingi upi hasa unaokuwa unautumia hapo? Kwamba mkopo unamaliza matatizo ya kifedha, na kuleta matokeo tofauti?

Kwa chochote ambacho kinakupa shida kwa sasa rafiki, sehemu ya kufanyia kazi ni moja, kwanza wewe mwenyewe, kuanzia kwenye mtazamo ulionao kwenye kile unachofanya.

Mtazamo wako kwenye biashara ni upi, je unajitumaje kwenye biashara hiyo, una ndoto zipi kubwa ambazo unazifanyia kazi? Unaweka ubunifu na kwenda zaidi ya wengine kwa kiasi gani?

SOMA; Usiitabiri Kesho Yako, Bali Itengeneze…

Kadhalika kwenye kazi yako, unaichukuliaje, je ile ni sehemu ya wewe kutumika na wengine na kupata tu fedha ya kusukuma maisha au ni sehemu ya wewe kutoa mchango kwa wengine na kufanya maisha yao kuwa bora zaidi.

Unapokuwa na changamoto ya kifedha, rudi kwenye mtazamo wako kifedha, je fedha kwako ni nini? Ni kitu cha kutumia kila unapokipata au kitu cha kusimamia na kupangilia vizuri? Je kwenye kila kipato unachoingiza kuna sehemu yoyote unayoweka akiba? Kwenye mpango wako wa kipato, una vyanzo vingapi unavyotegemea?

Rafiki unaona namna gani kazi ni kubwa kwa kuanzia kwako kabla ya kuiangalia dunia?

Wapo wengi ambao wanabadili biashara kila siku, wanakuambia hii hailipi na kwenda kuanza nyingine. Wakianza hiyo hawakai muda wanaenda nyingine. Huku ndiyo kukata matawi ukitegemea matunda tofauti. Utabadili biashara hata mia moja, lakini kama mtazamo wako juu ya biashara ni mbovu, kila biashara itakuwa ngumu na mbaya kwako.

Kwenye kazi ndiyo usiseme, kila kazi unayofanya unaona ni mbaya, unatafuta nyingine, siku chache za mwanzo hamasa iko juu, baada ya hapo kazi inaanza kuwa hovyo, tatizo siyo kazi, tatizo ni wewe.

Umewahi kuona mtu ambaye anaoa au kuolewa na kila mara mahusiano yake yanakuwa na matatizo? Mpaka watu wanaweza kusema ana bahati mbaya, kila mwanamke au mwanaume anayempata ni matatizo. Ambacho hawaoni ni kwamba, tatizo siyo la wale anaowapata, bali tatizo linaanzia kwenye mtazamo wake binafsi, huo ndiyo unawavutia wale wanawake au wanaume anaoingia nao kwenye mahusiano.

Rafiki, chukua neno langu hili, chochote unachopitia sasa, mzizi mkuu ni wewe mwenyewe, kama kuna mabadiliko yoyote unahitaji kufanya, hakikisha yanaanzia kwenye mtazamo wako, kwenye fikra zako. Hayo ndiyo yatakuwa mabadiliko yanayoleta matunda tofauti, mabadiliko mengine nje ya hapo yatakuwa ya kujifurahisha tu, kwani utaendelea kupata matokeo yale yale.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.