UKURASA WA 952; Jifunze Kwa Wengine, Lakini Usiige Maisha Yao…

By | August 9, 2017

Njia bora kabisa ya kujifunza kuhusu mafanikio, ni kupitia wale ambao wameshafanikiwa. Kabla hujaanza safari yoyote, ni vyema ukaangalia nani ambaye amefanikiwa kwenye safari hiyo na kujifunza mambo muhimu kutoka kwake.

Kupitia yeye utajua njia ipi nzuri kufuata na makosa yapi ya kuepuka kwenye safari hiyo. Kupitia wale waliofanikiwa, utaweza kupunguza makosa waliyofanya, utaweza kuchukua muda mfupi zaidi kuliko wao, kwa sababu huenda wao hawakuwa na mwongozo, ila wewe unao.

Lakini watu wamekuwa wanafanya kosa moja kubwa sana la kuiga kila kitu kwa wale watu ambao wamefanikiwa. Badala ya kujifunza na kuona wanafanyiaje kazi kwao binafsi, wanachukua kitu kama ambavyo kinafanywa au kimefanywa na wengine na kutaka kukifanya vile vile kwenye maisha yao.

Hili limekuwa haliwasaidii watu, zaidi ya kuwatesa na kujikuta wakishindwa kupata kile ambacho walikuwa wanakitaka.

SOMA; Watu Wenye Ushawishi Mkubwa Kwako Ni Hawa…

Huwezi kuiga kila kitu cha mtu halafu ukafanikiwa. Hii ni kwa sababu binadamu wote tunatofautiana, hata kama safari yetu ni moja, kila mtu ana njia yake ya kipekee, ambayo hakuna mtu mwingine anaweza kuipita. Sasa unapoiga wengine, unakazana kupita kwenye njia ambayo siyo yako, huku ukiacha njia yako. Unachagua mwenyewe kuweka ugumu zaidi kwenye mafanikio na kujihakikishia kutokufanikiwa.

Kuna vitu unaweza kuvichukua kwa watu kama vilivyo, mfano tabia fulani nzuri, mfumo fulani wa maisha, lakini lazima wewe mwenyewe ukae chini na kuboresha mfumo huo uendane na maisha yako, lazima uutengeneze upya, ili uendane na njia unayopita wewe. Na hapo ndipo unapoweza kufanya makubwa na kufanikiwa sana.

Mwanzoni wa safari yako ya mafanikio, unaruhusiwa kuiga kila kitu, kwa sababu mara nyingi wakati huo unakua hujijui hata wewe mwenyewe, unakuwa hujaijua njia yako. Hivyo unapojaribu njia mbalimbali za watu waliofanikiwa, mwenyewe unaanza kuona njia ipi inakufaa zaidi au wapi upo vizuri zaidi.

Ukishaanza kuona hilo, unajiboresha sasa na kuegemea ule upande ambao upo vizuri zaidi.

Utaweza kufanya hili kama kweli unajifunza kwa lengo la kuwa bora zaidi. Lakini kama utaanza kwa kuiga na kujisahau, utajikuta unakazana sana lakini hufanikiwi.

Hata kama utajifunza sheria za wengine nyingi kiasi gani, kuna wakati utafika na kuhitaji kutengeneza sheria zako mwenyewe. Sheria hizi zinaweza zisiwe mpya kabisa, lakini zinapaswa kuendana na maisha yako wewe, maono yako na mafanikio unayotaka.

Sheria inaweza kuwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, ila kwako unaiweka kuendana na kazi unayofanya wewe. Unafanya kwa kiasi gani, kama ni masaa basi mangapi, kama ni uzalishaji basi ni kiasi gani.

Sheria inaweza kuwa kujilipa sehemu ya kipato chako, kwako unaboresha zaidi, kiasi unachojilipa ni kipi, utakikuzaje, unakiweka wapi.

Lazima utengeneze mfumo wako wa maisha ya mafanikio, kwa kujifunza kutoka kwa wengine na kuboresha zaidi ili kuendana na wewe.

Usiige kila kitu na kutaka kukifanya kama wengine wanavyofanya. Kama ambavyo nimewahi kuandika, wakati mwingine unachoona kwa waliofanikiwa siyo kweli, yapo mambo ya ndani huwezi kuyaelewa, labda hawayasemi au hakuna anayetaka kuyajua.

Lazima uchague kujifunza na kuboresha zaidi, ili kila unachofanyia kazi, kiendane na wewe na kikuletee mafanikio makubwa na maisha bora yenye furaha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.