UKURASA WA 954; Ubobezi Huu Hautakusaidia Lolote….

By | August 11, 2017

Huwa nashangaa jinsi gani watu wanajua namna gani wengine wanapaswa kuendesha maisha yao, lakini hawana hata chembe ya wazo la namna gani maisha yao yanapaswa kwenda.

Karibu kila mtu ni mbobezi kwenye maisha ya wengine, kwa sababu tumekuza na kuishi kwenye jamii ambazo zinataka kila mtu awe sawa na wengine. Hivyo pale mtu anapochagua kuishi maisha ya tofauti na wengine, kila mtu hakosi neno la kumpa.

Na wakati mwingine mtu wala hajaishi tofauti, ila tu ameweka vipaumbele tofauti na wengine wanavyotegemea. Hawatamwacha bila ya maneno.

Umewahi kuona namna watu wanapangilia maisha ya wasanii na watu wengine maarufu? Utawasikia wakisema yule kakosea, hela zake angetumia hivi. Au huyu kakosea maisha yake angeyapeleka hivi.

Lakini watu hao ambao wapo tayari kutoa maoni kwenye maisha ya wengine, hawajui maisha yao yanaelekea wapi. Kile wanachosema kwa wengine, kwao hata hakipo kabisa.

SOMA; Kuwa Makini Unapoingia Kwenye Biashara Mpya, Hata Kama Umeshazoea Biashara…

Hapo ndipo unaposhangaa, inakuwaje mtu anatumia muda mwingi kubobea maisha ya wengine kuliko maisha yake binafsi?

Na hapo ndipo unagundua kwamba hawa ni aina ya watu ambao hawawezi kufanikiwa. Ni watu ambao wamechagua kuishi maisha ya kushindwa na kushangilia au kuzomea wengine

Nimekuandikia hili rafiki ili kukukumbusha kama bado umebaki kwenye ubobezi huo uondoke haraka. Unaweza kuwa ulishaondoka, lakini jamii nzima inayokuzunguka inafanya hivyo, na hivyo ni rahisi kuteleza na kurudi nyuma.

Kwa mfano umekuta watu wanajadili mahali kuhusu mtu fulani, unajikuta na wewe unasukumwa kutoa maoni yako kuhusu mtu yule.

Ninachotaka ufanye rafiki, kabla hujatoa maoni yoyote kuhusu maisha ya mtu yeyote, jiulize je maisha yako umeshayabobea vizuri?

Umeshajua kusudi la maisha yako na unalifanyia kazi kila siku?

Je unazo ndoto kubwa ambazo unafanyia kazi kwenye maisha yako?

Je umeipangilia siku yako vizuri kuanzia unapoianza mpaka unapoimaliza?

Je unavyo vipaumbele vya siku yako ambavyo unavifanyia kazi kwenye kila muda wa siku yako?
Nina uhakika baadhi ya maswali hapo yatakuwa HAPANA, kwa sababu yangekuwa ndiyo yote, usingejikuta kwenye hali kama hiyo, ya kushawishika kuanza kutoa maoni kuhusu maisha ya wengine.

Ungekuwa ‘bize’ kweli kweli kufanyia kazi vipaumbele vya siku yako husika kiasi kwamba usingejua hata hao wengine wanafanya nini na maisha yao.

Upande wa pili pia unahusika,

Kwamba kama kuna mambo unafanyia kazi, lakini watu wanakusema na kukupa maoni ya namna gani ya kufanya tofauti, usikimbilie kufanya kwa sababu kila mtu anasema ufanye kitu fulani.

Badala yake kaa chini na kujiuliza, je hao wanaokuambia ufanye tofauti, wanayajua maono na ndoto kubwa za maisha yako? Je wanalijua kusudi kubwa la maisha unayoishi?

Kwa sababu wengi wanaona nje, hivyo wanakimbilia kutoa maoni yao kwa mtazamo wa nje. Ila wewe pekee ndiye unayeona ndani, wewe ndiye unayeona wapi unaenda, wewe ndiye unayejua kusudi la maisha yako.

Kukimbilia kufanya kitu kwa sababu wengine wanasema, utafanya kila kitu kwenye hii dunia, kasoro tu ndoto zako. Kwa sababu vingi unavyoambiwa ufanye, siyo muhimu kwako na havikufikishi kule unakotaka kufika.

Usiogope kufanya kitu ambacho wengine hawakielewi, watu wote walioleta mabadiliko makubwa kwenye hii dunia mwanzoni hawakueleweka, tena wengine walihisiwa wana matatizo ya akili.

Mfano waliokuwa na maono ya kutengeneza ndege, kila mtu aliwashangaa na kuwacheka. Wakisema wameharibikiwa akili. Lakini wao hawakusikiliza maneno ya watu, waliendelea kufanyia kazi maono yao. Na mwisho wa siku wakashinda.

Iwapo utachagua kumsikiliza kila anayetoa maoni yake, jua ya kwamba unakuwa umechagua kuua ndoto kubwa za maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.