UKURASA WA 991; Kinachoota Haraka, Hupotea Haraka…

By | September 17, 2017

Sheria za asili ndiyo zinazoendesha maisha, kila kitu kinafuata sheria za asili. Hivyo kwa chochote unachofanya, hakikisha unafuata sheria za asili, au usiende kinyume na sheria za asili.

Kwa asili, chochote kinachoota na kukua haraka, huondoka haraka pia, huwa hakina maisha marefu.

Chukua mfano wa mimea miwili, mchicha na mbuyu.

Mchicha huota haraka sana, ndani ya siku chache baada ya kuutosha unakuwa umeshaota na hautachukua muda kukomaa. Baada ya hapo unakufa, hauna maisha marefu.

Lakini mbuyu unachukua muda mrefu kuota pale unapopandwa, na hata unapotoa mche, inachukua miaka mingi mpaka kuwa mti kamili. Lakini ukishakuwa mti, huishi kwa muda mrefu, huhimili vishindo na changamoto nyingi.

Kila Changamoto

Chochote kinachoota haraka hupotea haraka pia kwa sababu kinavyoota haraka kinakosa muda wa kutosha wa kuwa imara ili kukabiliana na changamoto mbalimbali. Nafikiri unaona wazi kwamba mizizi ya mbuyu ni tofauti kabisa na mizizi ya mchicha. Ikitoke mvua kubwa na yenye mafuriko, mchicha utazolewa kabisa wakati mbuyu utadumu.

Ndiyo hizi ni aina tofauti kabisa za mimea, lakini hata ndani ya mmea wa aina moja, mmea unaoota haraka haudumu kama ule unaochukua muda kuota.

SOMA; BIASHARA LEO; Ipe Biashara Muda, Usikimbilie Hatua Kubwa Haraka…

Hii ina maana gani kwetu?

Ina maana kwamba, chochote tunachofanya, tukazane kujijengea misingi imara ambayo itatuwezesha kudumu kwa muda mrefu. Tusikimbilie tu kukua na kupata zaidi, badala yake tukazane na msingi.

Iwe ni kwenye fedha, afya, mahusiano, kazi na hata biashara, mara zote huwa kuna njia za mkato za kukua na kupata zaidi, lakini hizi hazidumu kwa muda mrefu.

Hivyo badala ya kuweka nguvu kubwa kwenye kupata na kukua haraka, tukazane kujenga misingi. Misingi inapokuwa sahihi na imara, hakuna kinachoweza kukuzia kukua, na wala hakuna kitakachokuharibia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.