UKURASA WA 995; Mambo Yanapokwenda Vibaya, Una Machaguo Mawili…

By | September 21, 2017

Pamoja na malengo na mipango mikubwa unayoweza kuweka, siyo kila kitu kitakwenda kama ulivyopanga.

Na mbaya zaidi, mambo yatakwenda vibaya tofauti na ulivyopanga. Utakosa kile ulichotaka na wakati mwingine utapoteza ulichokuwa nacho.

Sasa katika hali kama hizi, una machaguo mawili pekee. Kile unachochagua katika haya mawili ndiyo kinaamua matokeo unayopata na hatua unazopiga.

Chaguo la kwanza ni kutaharuki, kupata tishio na hofu kubwa. Hapa unaona sasa kila kitu kimekwenda vibaya, mambo hayawezekani tena na hakuna mategemeo mazuri. Hatua unazochukua kwenye hali hii ya taharuki huwa siyo hatua nzuri. Huwa ni hatua za kukata tamaa au kuharibu zaidi ile hali ambayo mtu unakuwa unapitia.

Chaguo la pili ni kutulia, kutathmini hali uliyopo na kisha kuchukua hatua sahihi. Hapa unatulia na kuangalia kile ambacho umepitia, kuangalia hatua gani unazoweza kuchukua kwa pale ulipo sasa. Chaguo hili linakuwezesha kuchukua hatua ambazo ni bora, hatua zinazoweza kugeuza hali yoyote mbaya kuwa bora zaidi.

panic vs calm

Changamoto ni kwamba, ni rahisi sana kuchukua chaguo la kwanza la kutaharuki, hivyo ndivyo wengi wanavyofanya, na ndiyo tulichozoea. Hivyo kama mtu utataka kuweza kuchukua chaguo la pili, lazima ufanye kinyume na ulivyozoea.

SOMA; MAMBO 20 NILIYOJIFUNZA KWENYE KITABU HOW TO STOP WORRYING AND START LIVING.

Kwa mfano, pale unapopata matokeo ambayo hukutegemea kupata, usikimbilie kufanya maamuzi yoyote, usikimbilie kulalamika au kumlaumu yeyote, bali angalia pale ulipo sasa na kule unakotaka kwenda. Kisha angalia unawezaje kufika kule unakotaka kufika, kwa kuanzia hapo ulipo sasa.

Hata kama umekutana na matokeo mabaya kiasi gani, ipo hatua ya kuchukua, lipo jambo la kufanya, ambalo kama utatulia na kufikiri kwa makini, litakuwezesha kuchukua hatua bora zaidi.

Acha kutaharuki, tulia, tafakari, chukua hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.