UKURASA WA 996; Uhaba Wa Maisha…

By | September 22, 2017

Kanuni kuu ya uchumi ni kwamba, kitu kinapokuwa adimu, thamani yake inakuwa kubwa. Kunapokuwa na uhaba wa kitu, kile ambacho kinapatikana kwa shida, kinathaminiwa zaidi. Lakini kile ambacho kipo kwa wingi na kinapatikana kirahisi, thamani yake huwa inakuwa ndogo.

Kanuni hii ya uchumi tunaweza pia kuitumia kwenye maisha yetu, hasa pale tunapotaka kutengeneza maisha yenye maana kwetu.

Wote tunajua ya kwamba, miaka 100 ijayo, kila mtu anayesoma hapa atakuwa amekufa. Hii ina maana kwamba, maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana ukilinganisha na maisha ya dunia yenyewe.

Ulinzi

Kwa ufupi huu wa maisha, tunapaswa kuyathamini maisha zaidi. Tunapaswa kujua kwamba, chochote tunachochagua kufanya kwenye maisha yetu, tunakifanya huku muda wetu hapa duniani ukiwa unaendelea kupungua.

Swali ni je kile unachofanya sasa, kina thamani ya kutosha kulingana na maisha yako? Je kweli kile unachochagua kufanya kila siku kwenye maisha yako, kina hadhi ya muda mfupi ulionao hapa duniani?

Mara nyingi huwa hatupati muda wa kujikumbusha ufupi wa maisha yetu hapa duniani. Hatupati muda wa kutafakari kwamba kuna kifo kinatusubiri. Hivyo tunaweza kuchagua kufanya kila kitu kinachojitokeza mbele yetu.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kitu Kimoja Kibaya Ambacho Hatuwezi Kukikwepa, Na Jinsi Ya Kuishi Nacho Kwa Furaha.

Kifo kinatengeneza uhaba mkubwa kwenye maisha yetu, kitu ambacho kinafanya maamuzi yetu yawe yenye maana na thamani kubwa. Hivyo kila tunapofanya maamuzi muhimu ya maisha yetu, tujikumbushe uhaba huu wa maisha ili tuweze kufanya maamuzi yenye tija kwetu.

Watu wengi wanapokuwa kwenye siku za mwisho wa maisha yao, huwa hawajutii vitu walivyofanya na kuona wangefanya zaidi. Bali hujutia vile ambavyo hawakupata nafasi ya kufanya, kwa sababu hawakujua umuhimu wake kwa wakati huo.

Usisubiri mpaka unapofikia tamati ya maisha yako na kuanza kuona mengi uliyofanya hayakuwa na maana. Kaa leo na tafakari kila unachofanya, kama kina thamani ya kuiba maisha yako, fanya. Kama hakina thamani hiyo achana nacho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.