UKURASA WA 999; Unapoukaribia Ukweli, Hofu Inaongezeka…

By | September 25, 2017

Watu wengi hawapendi ukweli, kwa sababu ukweli haupendezi na wala hauwafurahishi watu. Ukweli haujaribu kumbembeleza mtu. Ukweli unakuwa ukweli, bila ya kificho, na wengi hawapendi hilo.

Hivyo ni kawaida hofu kuongezeka pale tunapoukaribia ukweli. Pale unapokaribia kuufikia ukweli, pale unapokaribia kufanya jambo ambalo ni sahihi, hofu inakuwa kubwa zaidi.

Hii ni kwa sababu unajua siyo wote watakubaliana nalo, na huenda wengi zaidi wakakupinga.

Mambo ya Kawaida

Unakuwa na hofu zaidi pale unapoanza kuyaishi maisha ya ukweli kwako, kwa sababu ni maisha ambayo ni ya kipekee, ambayo ni tofauti na ya wengine. Maisha ya aina hiyo yanakuweka kwenye nafasi ya kukosolewa na wengine, kuonekana kwamba unakosea kwa sababu hufanyi kama wengine wanavyofanya.

Hofu pia inaongezeka pale unapokuwa unafanya jambo sahihi, pale unapoanza kufanya kitu ambacho ni kikubwa, lakini ni sahihi. Unafikiria kama matokeo yasipokuja kama ulivyofikiri mambo yatakuwaje. Kwa upande wa pili, wengi wanaokosea huwa hawana hofu kabisa, wengi hujiamini kupita kiasi huku wakielekea kupotea.

SOMA; SIRI YA 32 YA MAFANIKIO; Zishinde Changamoto.

Ninachotaka kukuambia hapa rafiki yangu ni kwamba, unapoona hofu inaongezeka, usiogope na kuacha kufanya, bali fanya kwa sababu hofu hiyo ni dalili kwamba unalofanya ni sahihi na litakupeleka mbali zaidi. Ni dalili kwamba umeamua kuacha kuwa wa kawaida na unakwenda kuwa wa tofauti kabisa.

Unapoona hofu inaongezeka, hapo ndipo pa kuchukua hatua. Na kuchukua hatua ndiyo dawa pekee ya hofu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.