UKURASA WA 1013; Uaminifu Unavyojengwa…

By | October 9, 2017

Umewahi kusikia mtu anasema anapenda sana watu wamwamini lakini hawafanyi hivyo?

Au huenda wewe mwenyewe, kuna watu unataka sana wakuamini, lakini wao hawana imani juu yako. Labda ni wateja wako, mwajiri wako, mwenza wako, na hata watu wengine wanaokuzunguka.

Uaminifu ni kitu muhimu sana kwa mafanikio, kama watu hawakuamini, huwezi kufanikiwa. Kwa sababu hawatakuwa tayari kukupa kile ambacho unahitaji wakupe.

Kitu muhimu ambacho tunapaswa kufahamu ni kwamba uaminifu haujengwi kwa maneno, hata uwalilie watu kiasi gani kwamba wakuamini, hawatakuamini. Tena unavyokazana kuwaambia wakuamini, ndiyo wanazidi kupoteza imani juu yako.

Njia bora kabisa ya kujenga uaminifu ni kuahidi na kisha kutekeleza ahadi hiyo, kama ulivyoahidi, bila ya sababu yoyote.

Hapo nielewe vizuri sana, hasa sehemu ya mwisho ya BILA SABABU YOYOTE. Kwa sababu hakuna ambaye anashindwa kuahidi, lakini kutekeleza kama mtu alivyoahidi, bila ya sababu, ni wachache sana wanafanya hivyo.

Watu wana sababu tayari za kueleza kwa nini wameshindwa kutimiza ahadi walizoweka, hata kabla hawajaanza kufanyia kazi ahadi hizo.

Na cha kushangaza, watu hawajawahi kukosa sababu, wakikosa sababu zinazoelezeka, basi watakuja na sababu zisizoelezeka, sababu za kijinga kama shetani alinipitia. Unaweza kufikiria mtu inabidi awe mjinga kiasi gani kutoa au kupokea sababu ya aina hiyo.

SOMA; SIRI YA 30 YA MAFANIKIO; Uaminifu Unalipa Gawio Kubwa.

Hivyo muhimu rafiki, weka ahadi na timiza ahadi uliyoweka, bila ya kutoa sababu. Na kuweza kufanya hivyo, itakuhitaji kwenda hatua ya ziada, itakuhitaji kuumia, itakuhitaji kuingia gharama.

Lazima uwe tayari kupitia yote hayo, ili kutimiza ulichoahidi.

Na siyo kwamba ukishaahidi kitu kimoja ukakamilisha basi una haki na mamlaka ya kuwaambia watu wakuamini kwa sababu umetimiza, bado unahitaji kuendelea kuahidi na kutimiza, mara nyingi mno mpaka iwe tabia yako.

Mpaka ifike mahali kwamba ukiwaambia watu kitu, wanakuwa hawana wasiwasi wowote, kwa sababu umeshawadhibitishia, bila ya shaka yoyote kwamba kile unachosema ndiyo unachofanya.

Hili linawezekana, anza na ahadi ndogo ndogo, tekeleza, endelea kukua kwenye ahadi na tekeleza. Ukiwa mtu wa matokeo na siyo mtu wa sababu, watu wanakuamini na kuwa tayari kufanya kazi na wewe, kuwa tayari kukupa kile unachotaka. Na hapo ndipo mafanikio yako yalipo.

Ahidi kitu leo na kitekeleze, rudia hivyo kesho na kila siku ya maisha yako. Hivyo ndivyo uaminifu unajengwa.

Kumbuka kinyume cha hili pia kinafanya kazi, ukiahidi kitu na usitekeleze unaharibu uaminifu wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply