UKURASA WA 1015; Epuka Hali Hizi Tano Zinazokunyonya Nguvu Zako…

By | October 11, 2017

Umewahi kusoma kitu ukapata hamasa kubwa sana ya kuchukua hatua ili kuboresha maisha yako, lakini baada ya muda ile hamasa yote ikaisha kabisa na kujikuta unarudi pale pale ulipokuwa?

Najua hili kwa wengi kwa sababu nimekuwa naona watu wanaosoma vitabu au makala ninazoandika, wanahamasika kweli, wananipigia simu au kuandika ujumbe au email wakinieleza ni kwa namna gani wamekuwa hawajui mambo hayo muhimu, na kuamua kuchukua hatua kweli.

Lakini ukija kuwafuatilia baadaye, unakuta wameshasahau kabisa hata kile walichokuwa wamepanga kufanya. Wanakuwa wamerudi kwenye maisha yao ya kawaida na ile hamasa waliyokuwa nayo imepotea yote.

Kujilinganisha

Leo nimekukusanyia hali tano za kuepuka kama unataka kuendelea kuwa na hamasa.

Kwa sababu, hamasa ni nguvu na nguvu hiyo inapoisha, huwezi kuchukua hatua. Ni sawa na betri, inapokuwa na chaji inaweza kufanya makubwa, chaji ikiisha haiwezi kufanya kitu.

  1. Watu hasi.
Kama kuna watu ambao kila unachowaambia hawakosi kitu cha kukosoa na kuonesha haiwezekani, waepuke haraka sana. Usiwaambie mambo yako au kaa nao mbali kabisa. watu hawa ni watu sumu, wanakunyonya nguvu na huwezi kuchukua hatua kabisa.
 
      2. Wivu.
 
Kama unawaangalia wengine na kuona wamepiga hatua na kuona wivu, kwa nini wao wameweza na wewe hujaweza, huwezi kuchukua hatua. Badala yake utaishia kuwachukia waliochukua hatua na kuomba kimoyomoyo wakutane na ugumu kwenye maisha yao.
 
NB; Wivu ni wivu, hakuna wivu mzuri wala mbaya. Unaweza kuhamasika kupitia wengine waliokuzidi, ukawapenda na kujifunza kutoka kwao, au ukawaonea wivu. Wivu unakunyonya nguvu na huwezi kuchukua hatua.
 
      3. Chuki.
 
Chuki yoyote uliyonayo kwenye maisha yako, itakuzuia wewe kuweza kuchukua hatua na kufanikiwa. Hata kama chuki haihusiani na kile unachofanya, uwepo wa chuki rohoni mwako ni kikwazo kwako. Chuki inakunyonya nguvu na hutaweza kupiga hatua.
 
     4. Habari hasi.
 
Habari yoyote hasi, inakunyonga nguvu zako. Kama unaianza siku yako kwa habari, kwa hakika siku hiyo haiwezi kuwa bora. kwa sababu sehemu kubwa ya habari ni hasi, zimejaa hofu ya kukufanya wewe uone dunia inazidi kuwa mbaya. Ukiwa mfuatiliaji mzuri wa habari, hutakuwa na nguvu ya kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
  1. Mitandao ya kijamii.

Hii ndiyo hatari kabisa kwenye kunyonga nguvu, kwa sababu kwanza inachukua muda mwingi, mtu anajikuta kila wakati anachungulia kuona nini kinaendelea. Pili kile anachoangalia siyo salama, labda ni kujilinganisha na maisha ya wengine, ambayo kwa sehemu kubwa ni ya kuigiza, au kukutana na habari na taarifa hasi, ambazo hata hazijadhibitishwa kwa sehemu kubwa. Mtu yeyote mwenye hofu zake anaweza kuwajaza hofu watu wengi kupitia mitandao hii.

Unahitaji kuwa makini sana kuweza kulinda nguvu zako na hamasa yako ya kuchukua hatua ili kufanikiwa. Linda sana akili yako, ilishe vitu vizuri, vitu vinavyokuhamasisha na kukuonesha hatua za kuchukua.

Hii haimaanishi upuuze kila kinachoendelea, badala yake kipaumbele chako cha kwanza kiwe kwenye kuchukua hatua na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Hayo mengine yadhibiti sana, chukua yale muhimu pekee na yachukue ukijua yana madhara pia.

Ila wivu, chuki na habari hasi, achana navyo kabisa. utakuwa bora zaidi bila ya vitu hivyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply