UKURASA WA 1018; Ubaya Na Uzuri Wa Fedha Uko Wapi?

By | October 14, 2017

Fedha, neno ambalo likitajwa kila mtu anapata hisia zake. Wapo ambao wanaona ni kitu kizuri na bora sana, kitu ambacho wapo tayari kukifanyia kazi maisha yao yote.

Wapo ambao neno hilo likitajwa wanapata simanzi, wanaona ni kitu ambacho kimeharibu kabisa maisha yao. Kitu ambacho kimewatenganisha na wale wa muhimu, kuharibu afya zao na hata kubomoa mahusiano yao.

Swali ni je, fedha ni nzuri au mbaya?

Nilishajibu swali hili kwenye maeneo mbalimbali, kwenye makala za fedha na hata kwenye semina za fedha.

Jibu ni kwamba, fedha siyo nzuri wala siyo mbaya, bali fedha ni fedha. Tunaweza kusema pia kwamba fedha ni nzuri na pia fedha ni mbaya.

Sasa swali muhimu la leo ni uzuri na ubaya wa fedha uko wapi?

Na hapa ndipo muhimu kuangalia ili tujue sehemu sahihi ya fedha, tuweze kuipa uzito unaostahili.

Tuanze na swali; je noti ya shilingi elfu kumi ni nzuri au ni mbaya?

Ukichukua noti hiyo ya shilingi elfu kumi, ukanunua chakula na kwenda kula na familia yako, noti hiyo ni nzuri mno, imefanya jambo kubwa na la maana.

Ukichukua noti hiyo hiyo, ukaenda kununua madawa ya kulevya kwa sababu ya kujipa raha, itakuwa imekuwa mbaya mno, kwa sababu imefanya jambo linaloharibu afya yako na kuvunja mahusiano yako na wengine.

Katika hali hizo mbili, noti ni ile ile, elfu kumi, lakini yaliyofanyika ni tofauti.

Hivyo unaweza kuona kwa nini fedha siyo nzuri wala siyo mbaya.

Uzuri na ubaya wa fedha upo kwa yule anayezimiliki fedha.

Kama fedha zitakuwa kwenye mikono ya mtu mbaya, mtu ambaye haishi kwa misingi mizuri, fedha hizo zitakuwa hatari sana kwake na kwa kila anayemzunguka.

Lakini kama fedha zitakuwa kwenye mikono ya mtu mzuri, mtu ambaye anaishi kwa misingi mizuri, fedha hizo zinakuwa baraka kwake na kwa wanaomzunguka.

Fedha ni kichocheo cha tabia ambayo tayari ipo ndani ya mtu. Hata wale wanaosema mtu amebadilika baada ya kupata fedha, siyo kweli. Fedha haiwabadilishi watu, bali fedha inafanya tabia za watu ziwe rahisi kuonekana.

Hivyo usiache kutafuta fedha, tena nyingi sana kwa kigezo kwamba wengine wamezipata na maisha yao kuharibika. Fedha haina nguvu ya kuharibu, bali ni kichocheo kizuri cha chochote kilichopo ndani ya mtu.

Na hili linafanya iwe muhimu sana kwako kujijengea misingi sahihi, ili hata unapokuwa na fedha nyingi, maisha yako yaendelee kuwa bora zaidi na wengine wanufaike zaidi na uwepo wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.