UKURASA WA 738; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…

By | January 7, 2017

Sasa hivi karibu kila kitu kimefanywa kuwa demokrasia.

Zile enzi za kitu kimoja kukubaliwa na watu wote zimeshapitwa na wakati na hazitarudi tena.

Kuanzia kwenye biashara, kazi, huduma na hata maisha kwa ujumla, hakuna kitu kimoja ambacho kinaweza kukubalika na kila mtu. Ila kila kitu kina watu wake sahihi.

Lakini watu wengi, hasa wanaofanya biashara wamekuwa hawaelewi hili, wamekuwa waking’ang’ana kuhakikisha kila mtu anakuwa mteja wao, wanapoteza muda, nguvu na fedha na mbaya zaidi kuwapoteza watu sahihi.

Kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, jua ya kwamba siyo kila mtu atakubaliana na wewe, huwezi kumshawishi kila mtu.

Bali kuna watu sahihi kwa kile unachofanya, watu wanaoamini sawa na unavyoamini wewe, wanaotaka kufika kule unakotaka kufika wewe. Hawa ndiyo watu sahihi kwako na utaweza kufika nao mbali sana.

SOMA; Watu Wanakuangalia Zaidi Ya Kukusikiliza….

Kwenye biashara, chagua aina ya wateja ambao unahitaji kuwahudumia, ambao upo tayari kuwapa mahitaji yao, kutatua matatizo yao na kufanya maisha yao kuwa bora. Komaa na wateja hawa na achana na wengine wote.

Usipoteze muda kukimbiza wale ambao hawaendani na biashara yako, kwa sababu hutawapata na mbaya zaidi utashindwa kuwahudumia vizuri wale ambao ni sahihi kwako na hivyo kuwafanya waondoke.

Lakini kama utawahudumia vizuri wale ambao ni sahihi kwa biashara yako, wataridhika na watawafanya wengine nao waje kwako.

Wengi wamekuwa hawafanyi hili kwa sababu wamekuwa wanataka kufikia wingi kwa haraka. Kwa sababu ukianza na wale ambao ni sahihi, huwa wanakuwa wachache. Lakini kadiri unavyokwenda, wanakuwa wameongezeka kwa sababu wachache wanapopata mazuri, wanawavutia wengi zaidi nao kuja kupata mazuri.

Usidanganyike na kutafuta wingi kwa kuwaendea ambao siyo sahihi, watafute wale ambao ni sahihi na utaweza kuwafikia wengi zaidi ambao nao ni sahihi.

Huhitaji kila mtu, unahitaji watu sahihi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 738; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…

  1. Pingback: UKURASA WA 972; Pamoja Na Changamoto Zao, Maisha Yetu Hayana Maana Bila Ya Watu… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.