UKURASA WA 742; Kufanya Mara Moja Moja Na Kufanya Kila Siku…

By | January 11, 2017

Kuna vitu ambavyo huwa tunafanya mara moja moja kwenye maisha yetu, halafu kuna vile vitu ambavyo huwa tunavifanya kila siku. Katika vitu hivi vya aina mbili, unafikiri vipi vyenye nguvu kwetu? Vipi ambavyo vinayajenga maisha yetu?

Maisha yetu yapo pale yalipo sasa, kutokana na tabia ambazo tunazo, na tabia yoyote inajengwa na vitu ambavyo tunavifanya kila siku. Hivyo basi maisha yetu yapo pale yalipo sasa kutokana na vitu ambavyo tumechagua kufanya kila siku. Hii ina maana kuwa kama tunataka kubadilika, kama tunataka kutoka hapa tulipo sasa, basi tunahitaji kubadili yale mambo tunayofanya kila siku.

Wakati mwingine watu huwa wanapata hamasa, na kuanza kufanya mambo mazuri, lakini wanayafanya mara moja moja, sasa kufanya kitu mara moja moja hakukuwezeshi wewe kufanikiwa au kupata matokeo mazuri. Kufanya mara moja na kuacha hakuna faida kubwa kwako. Faida unaipata pale unapofanya kwa kujirudia rudia, kwa kufanya kila siku na hatimaye inakuwa tabia na inakuwezesha kufanya makubwa na kufanikiwa.

Hivyo hebu angalia maisha yako, kwa hapo ulipo sasa, ni mambo gani ambayo umekuwa unafanya kila siku, ukichunguza kwa undani kama bado utagundua kuna mengi unayafanya kwa kurudia kila siku, labda kutokuanza siku yako mapema, kukosa umakini kwenye kile unachofanya na mengine.

SOMA; Wakati Sahihi Wa Kufanya Mabadiliko Ni Huu…

Pia angalia kule unakotaka kufika na maisha yako, na jiulize ni mambo gani unahitaji kufanya kila siku ili kuweza kufika kule. Angalia hatua za kuchukua kila siku na zichukue kila siku utaona mabadiliko.

Usiwe mtu wa kukurupuka na kufanya mambo mara moja moja ukitegemea mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Mabadiliko huwa hayaji hivyo hata siku moja. Mabadiliko na mafanikio yanatokana na vitu vidogo vidogo unavyofanya kila siku.

Anza sasa na fanya kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.