UKURASA WA 752; Ujuzi Na Mtazamo…

By | January 21, 2017

Tunapotafuta watu wa kuwaajiri au wa kushirikiana nao kwenye mambo mbalimbali ya maisha yetu, mara nyingi tumekuwa tunaangalia ujuzi. Ndiyo maana matangazo ya kazi utaona yameandika awe ana ujuzi fulani, au awe na elimu fulani. Na hata watu wanapokuwa wanaweka mipango yao mbalimbali ya maisha, inayowahusisha wengine, huwa wanaweka sana ujuzi. Utasikia mtu anasema nataka mke au mume ambaye ni mwalimu, au daktari au ujuzi mwingine wowote.

Hapa ndipo watu wengi wanapokosea na kupotea kwenye kuchagua watu kwa lolote wanalohitaji kufanya nao.

SOMA; Maswali Matatu Muhimu Kujiuliza Kabla Ya Kuchukua “RISK”…

Watu wana ujuzi ambao unaweza kufundishwa wakati wowote ule. Lakini muhimu zaidi watu wana mtazamo, wana tabia ambazo wanazo ambazo haziwezi kubadilishwa kwa haraka. Ninachosema ni kwamba kila mtu ana mtazamo wake kuhusu maisha, na ana tabia fulani ambazo zimeshakuwa sehemu ya maisha yake. Hata ufanye nini wewe kama wewe huwezi kubadili mtazamo huo au tabia hizo.

Unaweza kumfundisha mtu ujuzi wowote unaoutaka wewe, lakini huwezi kubadili mtazamo wake na tabia zake kama unavyotaka wewe. Hivyo basi tunahitaji kufanya mabadiliko kwenye vigezo tunavyotumia kuchagua watu kwa mambo tunayohitaji kufanya. Badala ya kuangalia ujuzi pekee, tuanze na kuangalia mtazamo wa watu hao na tabia zao pia.

Unapokuwa na watu wenye mtizamo na tabia sahihi, unaweza kuwafundisha chochote ambacho ni muhimu kwao kujua ili kuweza kupata matokeo bora.

Ni rahisi sana kufundisha ujuzi au mtu kufundishwa ujuzi fulani. Ni vigumu mno kwa mtu kufundishwa mtazamo au tabia nzuri. Hivyo badala ya kuchagua njia ambayo utakusumbua, badili vigezo vyako vya kukubaliana na mtu.

Hata inapofikia wakati unashindwa kuendelea na mtu, labda i mfanyakazi unamfukuza, mfukuze kwa mtazamo na tabia zake na siyo kwa ujuzi wake. Kwa sababu ujuzi unaweza kubadilishwa, ila mtazamo na tabia ni vigumu wewe kuweza kuvibadilisha.

Warren Buffet, mwekezaji bilionea amewahi kunukuliwa akisema kwamba kwenye kuajiri angalia vitu vitatu; uaminifu, akili na nguvu, kama uaminifu hakuna, hivyo vingine viwili vitakumaliza. Yaani kama mtu ana akili na ana nguvu, halafu siyo mwaminifu, atakumaliza, kwa sababu atatumia sifa hizo mbili vibaya na utakuwa kwenye matatizo.

Kuwa makini na wale watu ambao unashirikiana nao, angalia zaidi tabia zao na mitazamo yao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.