UKURASA WA 800; Dawa Moja Inayotibu Matatizo Yako Yote….

By | March 10, 2017

Kama ipo dawa moja ambayo inaweza kutibu matatizo yako yote,

Inaweza kutibu matatizo yako ya kiafya na kuhakikisha unakuwa na afya bora sana, maradhi hakuna.

Inatibu matatizo yako ya kifedha na kukuondoa kwenye madeni na uhaba wa kipato.

IMG-20170227-WA0005

Inaweza kutibu matatizo yako ya kikazi, kuondoa msongo wa mawazo unaotokana na kazi zako za kila siku.

Inaweza kuondoa matatizo yako ya kibiashara, kwa kukuwezesha kuendesha biashara zako vizuri na kuzishinda changamoto.

Inaweza kuondoa matatizo yako ya kimahusiano na kindoa na kujenga ushirikiano mzuri na wale ambao ni muhimu kwao.

Je ungelipa kiasi gani uweze kupata dawa hii?

Ungekuwa tayari kiasi gani kuhakikisha unapata dawa hii, ambayo ukiinywa tu, maisha yako yanaanza kubadilika, na kuwa bora sana.

SOMA; Dawa Kamili Ya Hofu Ni Hii…

Nakumbuka mwaka 2010 kilitokea “KIKOMBE CHA BABU” ambacho kilidhaniwa kuwa ni dawa ya maajabu, yenye uwezo wa kutibu kila aina ya ugonjwa. Kikombe hichi hakikuwa ghali, kilikuwa shilingi 500 pekee, fedha ndogo sana ambayo hakuna anayeweza kuikosa, hata ukimwomba yeyote anakupa. Changamoto ilikuwa ni kwamba, mpaka ufike kikombe kilipo, ulihitaji kutumia gharama kubwa mno. Na kulingana na unapotokea, basi gharama zilikuwa kubwa zaidi.

Sasa leo nataka nikuambie nimekuja na KIKOMBE kipya, kikombe hichi kinaweza kutibu siyo tu magonjwa, bali matatizo yoyote unayopitia kwenye maisha yako. Kikombe hichi hakina gharama yoyote ya kukilipia, ila kinahitaji juhudi nyingi kuweza kukipata na kukitumia kwenye maisha yako.

Kikombe hichi ni NIDHAMU. Amini usiamini, sasa hivi anza kuangalia matatizo yanayokusumbua, yote yalianza na ukosefu wa nidhamu. Usiniamini mimi haraka, wewe jipe muda na anza kukagua kila hali unayoipitia.

Kama upo kwenye madeni, kuna wakati ulikosa nidhamu, na kuanza kuwa na matumizi makubwa kuliko mapato yako. Kuna wakati uliamua kununua vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako. Na muhimu zaidi umeshindwa kujiongoza na kuweza kuongeza kipato chako, licha ya kuwepo na njia nyingi za kufanya hivyo.

Kadhalika kwenye afya, kama unaumwa, wewe angalia tu, kuna wakati hukujali afya yako, ulikula hovyo au hukula kwa wakati, hukufanya mazoezi, hukujilinda na kadhalika.

Hivyo pia kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla. Hakuna biashara inayokufa au kushindwa kuendelea kama mwendeshaji hajakosa nidhamu. Unatoa fedha kwenye biashara kwa matumizi yako binafsi. Au kwa kuwa biashara ni yako unaiendesha unavyotaka wewe, na kusahau wateja wanataka nini.

Kunywa kikombe cha nidhamu leo rafiki yangu, na utaondokana na matatizo mengi kwenye maisha yako. Nidhamu ni uhuru, nidhamu ni kuweza kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi. Nidhamu ni kufanya kile ambacho ulipanga kufanya kwa wakati uliopanga kufanya. Nidhamu ni kutokubali chochote kikuzuie au kikurudishe nyuma.

Kikombe kipo ndani yako, sijakuambua uje kwangu ndiyo unywe, au uende sehemu maalumu, anza kukinywa sasa, kwa mambo madogo madogo na utaweza kunufaika zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.