UKURASA WA 859; Ujasiri Unahitajika Pia…

By | May 8, 2017

Hakuna kitu utakachofanya, wakosekane watu wa kukukosoa au kukupinga. Pamoja na juhudi kubwa unazoweka, wapo ambao watasema unachofanya siyo sahihi, wengine watasema unapoteza muda, na wapo watakaokushauri kipi hasa ufanye.

IMG-20170217-WA0003

Hivyo, kitu kikubwa sana unachohitaji, ni ujasiri, kwenye jambo lolote lile ambalo utaamua kufanya. Kwa sababu bila ujasiri, hutaweza kwa upinzani utakaokutana nao. Kuanzia kwenye changamoto, wewe mwenyewe na hata wale wanaokuzunguka.

Unahitaji ujasiri wa kuwaambia watu hapana na kuendelea kuweka juhudi, hata kama watu hao ni wale unaowaheshimu sana.

Unahitaji ujasiri wa kupingana na wale ambao wamekufundisha njia sahihi ya kufanya, au ambao wanaamini ndiyo wako sahihi zaidi.

Pia unahitaji ujasiri wa kukaa mbali na wale ambao watakukasirisha, hasa pale baada ya kuweka juhudi kubwa na kupata kitu, wale ambao hawakuhusika kabisa watakapojitokeza na kusema bila wao usingeweza, hivyo lazima uwashukuru sana.

SOMA; Siri Ya Kupata Ujasiri Wa Kuuliza Chochote…

Hata baada ya kupata, wapo pia watakaokuambia ulikutana na bahati, ulibahatisha au umependelewa. Pamoja a maumivu unayojua uliingia, wapo ambao watachukulia ni urahisi sana. Licha ya yote hayo, unahitaji ujasiri wa hali ya juu sana, kuyavuka na kuendelea na mapambano.

Mafanikio ni rahisi unapoyaona kwa nje, ila kama hujawahi kusimamia jambo mpaka likakamilika, huwezi kujua ujasiri ambao unahitaji ili kupata unachotaka. Siyo tu kuweka kazi na juhudi, ambayo ni muhimu, bali ujasiri wa kuvuka kila kitakachoibuka dhidi yako, utakusaidia sana kupata unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.