UKURASA WA 864; Usipunguze Bei, Ongeza Thamani…

By | May 13, 2017

Watu wengi wanapoingia kwenye biashara, huwa wanaangalia njia rahisi ya kuwazidi washindani wao. Na njia rahisi kabisa, isiyohitaji ubunifu wa aina yoyote ile ni kupunguza bei. Lakini kama ilivyo kwa vitu vingi rahisi, huwa vina madhara, na madhara ya kupunguza bei ni makubwa sana kwenye biashara yoyote ile. Kwani kupunguza bei hupelekea hata huduma zinazotolewa kuwa za kiwango cha chini, ili kuweka gharama chini. Na mbaya zaidi, unapopunguza bei, mshindani wako naye anaweza kupunguza zaidi yako, hapo ndipo mnapojikuta kwenye mbio za kuporomoka kibiashara.

Njia nzuri ya kujitofautisha na washindani wako kibiashara, bila ya kupunguza bei na kuweza kupata wateja wengi zaidi, ni kuongeza thamani. Kitu kile kile ambacho mteja anapata kwa wengine, kiongezee thamani, na uza kwa bei sawa, au wakati mwingine ya juu kidogo. Hakuna mtu ambaye hapendi thamani, hivyo bei zinapokuwa sawa na wewe una thamani zaidi, wateja wengi watakuja kwako. Na wale wanaokuja, watawaambia wengine wengi zaidi na kuwa na wateja wengi.

Watu wengi wanaposikia thamani hufikiri ni mpaka uweke vitu vikubwa sana. Lakini huo siyo ukweli, kitu chochote ambacho mteja anajali zaidi, ni thamani ya kutosha. Inaweza kuwa namna anavyohudumiwa, anavyosikilizwa na anaposaidiwa akipata changamoto. Inawezekana ni kusafirishiwa bidhaa pale baada ya kununua. Inawezekana ni kupewa kitu cha nyongeza baada ya kununua. Chochote kile ambacho mteja atajali, na kitamfanya awe bora zaidi ni thamani.

SOMAJinsi Ya Kuwafundisha Watoto Wako Thamani Ya Fedha….

Hivyo unapofikiria kuongeza wateja zaidi kwenye biashara yako, usikimbilie kupunguza bei, bali jiulize ni thamani gani unaweza kuongeza kwa wateja wako zaidi? Kwa njia hii utaona mengi ya kufanya na kuweza kuyaongeza.

Pia unapopanga kuongeza bei, hakikisha kuna thamani unaongeza zaidi. Kuweka bei kubwa kwa thamani ile ile ya mwanzo, inaweza kumfanya mteja aone kama anaibiwa, na kutafuta ambapo atapata kwa bei aliyozoea. Ila unapoongeza thamani, mteja anaona ni sahihi kuongeza bei kwa sababu anafaidi zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.